"Naumia, Mniombee" Zuchu aumia goti baada ya kuhusika kwenye ajali

Muhtasari

• Zuchu alipakia video fupi inayoonyesha daktari akiweka nyuzi kwenye jeraha ambalo alipata kufuatia ajali hiyo.

•Zuchu hata hivyo ameonyesha  nia kubwa ya kuenda kufanya shoo yake ya Nigeria bila kujali maumivu anayoyapata.

Image: FACEBOOK// ZUCHU

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu anaendelea kuuguza jeraha la goti baada ya kuhusika kwenye ajali ndogo usiku wa Jumamosi.

Zuchu alitangaza kuhusu ajali hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter. Alipakia video fupi inayoonyesha daktari akifunga jeraha ambalo alipata kufuatia ajali hiyo kutiumia nyuzi.

Masaibu hayo yalimpata Zuchu huku ikiwa imesalia siku moja tu afunge safari ya kuelekea Nigeria kwa ziara ya kikazi.

"Nimepata Ajali ndogo iliyo umiza goti langu jana siku moja kabla ya safari yangu kwenda kuperform Kwenye show Ya Muhimu kwangu nchini Nigeria .Kughairi shoo ni mojawapo wa uamuzi mmoja mgumu zaidi siwezi kama msanii. Leo ndio nimejua,"  Zuchu aliandika.

Ajali hiyo ilimuweka msanii huyo wa WCB katika njia panda ikiwa bado atatumbuiza nchini Nigeria kama alivyopanga au anafaa kuahirisha.

Zuchu hata hivyo ameonyesha wazi kuwa ana nia kubwa ya kuenda kufanya shoo hiyo bila kujali maumivu anayoyapata. Amewasihi watukumkumbuka katika maombi huku akisema kuwa anaumia sana.

"Meneja wangu huwa ananiambia Afya ni muhimu ila najua ntajiskia vibaya zaidi kutaka kucancell kwenye show kama hii naona bora nikapambanie stagini kwa hivyo mniombee .Nimeumia na nimechanganyikiwa," Zuchu alisema.

Asubuhi ya Jumatatu msanii huyo kutoka Zanzibar alifichua kuwa yupo katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa  Bole nchini Ethiopia. Hata hivyo hakufichua ikiwa alikuwa anaabiri ndege ama alikokuwa anaelekea.

"Nipo nchini Ethiopia kwa sasa na ninachosikia ni Bongofleva tu," Zuchu aliandika.

Zuchu anaaminika kuwa mwanamuziki mkubwa zaidi wa kike nchini Tanzania  kwa sasa. Malkia huyo wa muziki ameendelea kutesa hasa tangu alipojiunga na Wasafi mwaka wa 2020.