Mpenzi mpya huponya moyo uliovunjwa, si muda!- Ex wa Baha, Georgina Njenga awashauri wanadada

Mzazi huyo mwenza wa Baha amekanusha wazi kwamba ni muda ambao huponya moyo ulioumizwa.

Muhtasari

•Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 amebainisha kuwa kupata mpenzi mpya baada ya kuvunjwa moyo kunaondoa uchungu.

•Georgina alikiri kuwa yuko tayari kujaribu ndoa tena hata baada ya jaribio la kwanza la muigizaji Tyler Mbaya kufeli miezi kadhaa iliyopita.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Siku ya Jumapili asubuhi, mtayarishaji maudhui Georgina Njeri Njenga alishiriki na mashabiki wake vidokezo kuhusu jinsi ya kuponya moyo ulioumizwa.

Katika ushauri wake mfupi ulioelekezwa kwa wanawake, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alibainisha kuwa kupata mpenzi mpya baada ya kuvunjwa moyo kunaondoa uchungu.

Mpenzi huyo wa zamani wa aliyekuwa muigizaji wa Machachari, Tyler Mbaya almaarufu Baha, alikanusha wazi kwamba ni muda ambao huponya moyo.

"Sio wakati ambao huponya moyo uliovunjika, ni mwanaume mpya dada," Georgina aliandika kwenye video yake ambayo alichapisha kwenye Instagram.

Ushauri huu unakuja siku chache tu baada ya mama huyo wa binti mmoja kukiri kuwa yuko tayari kujaribu ndoa tena hata baada ya jaribio la kwanza la muigizaji Tyler Mbaya kufeli miezi kadhaa iliyopita.

Alhamisi iliyopita, Bi Georgina aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram ambapo alifunguka kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake, mahusiano na mambo mengine.

Katika mojawapo ya maswali, alitakiwa kujibu iwapo anawaza kujitosa tena kwenye ndoa baada ya uhusiano wake na Baha kugonga mwamba mapema mwaka huu.

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 pia aliulizwa kama ana nia ya kupata mtoto mwingine katika siku zijazo.

“Utawahi kuolewa tena?? Au kuzaa tena?,” shabiki mmoja aliuliza.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Katika majibu yake, alidokeza kwamba ana mpango wa kujaribu ndoa tena katika siku zijazo lakini hana uhakika kuhusu kupata watoto zaidi.

"Kuolewa, ndio .. kuhusu watoto, hapana. Lakini huwezi kujua maishani,” Georgina alijibu.

Wakati alipoulizwa kuhusu anachopendelea kati ya kuolewa na kuwa bila mchumba, alibainisha kuwa chaguzi zote mbili zina madhara yake.

"Zote ziko na madhara.. chagua mapambano yako kwa busara," alisema.

Georgina alithibitisha kuachana na mzazi mwenzake Tyler Mbaya takriban miezi minne iliyopita ambapo pia alifichua kuwa tayari yuko kwenye uhusiano mwingine.

Alifunguka kuhusu mwisho wa uhusiano wao alipokuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi kingine cha maswali na majibu kwenye Instagram.

"Wengi wenu mnauliza swali hili. Hii ni mara ya mwisho nitajibu. Tuliachana na niko kwenye uhusiano mpya na mwanamume wangu mpya,” Georgina alisema.

Kabla ya Georgina kuthibitisha kutengana kwao, mengi ya kutatanisha yalikuwa yametokea katika uhusiano wao yakidokeza kwamba ulikuwa karibu kuisha.