Mrembo aliyeonekana akimbusu na kumpapasa kimapenzi mume wa Zari avunja kimya, aeleza ukweli

DJ Alisha alionekana kumpapasa kimahaba mume huyo wa Zari na hata kumbusu mashavuni wakati wakiendelea na safari yao.

Muhtasari

•Video za Shakib  akijivinjari na DJ Alisha zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hisia mseto.

•DJ Alisha amefunguka kuhusu ukweli halisi wa video hiyo ambapo alifichua kuwa ilirekodiwa miaka mingi iliyopita.

Shakib Cham akijivinjari na DJ Alisha
Image: HISANI

Baadhi ya video za mume wa mwanasosholaiti Zari Hassan, Shakib Cham Lutaaya akijivinjari na mcheza santuri maarufu wa kike wa Uganda, DJ Alisha zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hisia mseto.

Katika video moja, mfanyabiashara huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 31 anaonekana akiwa amemshika mcheza santuri huyo mrembo huku wakiwa ndani ya gari moja ambapo walikuwa wakifurahia muziki aina ya hiphop.

DJ Alisha pia anaonekana kumpapasa kimahaba mume huyo wa Zari na hata kumbusu mashavuni wakati wakiendelea na safari yao.

Video hiyo iliyoibuka siku ya Alhamisi jioni baada ya mke wa Shakib, Zari Hassan kuonekana akiwa ameshikana mikono kimahaba na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz ilizua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii huku mashabiki wengi wakidai kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 31 alikuwa akilipiza kisasi.

DJ Alisha hata hivyo alikuwa mwepesi kufunguka kuhusu ukweli halisi wa video hiyo ambapo alifichua kuwa ilirekodiwa miaka mingi iliyopita.

"Hiyo ni video ya zamani. Miaka mingi iliyopita,” DJ Alisha alisema kupitia mtandao wa Twitter na kuambatanisha taarifa yake na emoji za kucheka.

Mcheza santuri huyo mrembo hata hivyo hakufichua uhusiano wake halisi na Shakib au ni nini hasa kilitokea mnamo siku video hiyo iliporekodiwa.

Video nyingine ambayo pia ilisambazwa sana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii iliwaonyesha Shakib na DJ Alisha wakiwa pamopja kwenye sehemu moja ya burudani ambapo walionekana kuburudika. Katika video hiyo, mcheza santuri huyo alionekana akicheza densi akiwa amekaa chini huku Shakib akiwa amesimama nyuma yake.

Hapo awali siku ya Alhamisi, video inayomuonyesha mwanasosholaiti Zari Hassan akitembea huku akiwa ameshikana mikono na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Bosi huyo wa WCB alikuwa wa kwanza kuchapisha video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alimtambulisha mama huyo wa watoto wake wawili kama dada yake.

“Mimi na dada @zarithebosslady,” Diamond aliandika chini ya video hiyo.

Video hiyo iliyosambazwa ilizua hisia mseto kutoka kwa wanamtandao tofauti ambao walitaka kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

Zari alijibu, “aaai, nimekufa.”

Shakib pia alijibu kwa njia yake mwenyewe isiyo ya moja kwa moja ambapo alidokeza kwamba hajafurahishwa na maendeleo ya hivi punde.

"Watu wenye nia safi wapate watu safi wenye nia safi," alichapisha kwenye instastories zake.

Pia alishiriki, "Mitandao ya kijamii inakufanya uvutie watu ambao unapaswa kuwaombea."

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 31 pia alifuta picha nyingi zinazomuonyesha akiwa na Zari kwenye ukurasa wake wa Instagram ikiwa ni pamoja na ile ya hivi punde aliyoshiriki mnamo siku ya wapendanao.