Mtangazaji wa Wasafi, Diva aanika majibu ya HIV baada ya kudaiwa kuwa +ve, afunguka madai ya ugumba

Mwijaku alidai Diva hana uwezo wa kupata mtoto, hiivyo mumewe kamfukuza kwa kutomzalia.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, Diva alilazimika kuanika matokeo ya vipimo vyake vya UKIMWI baada ya kuwepo kwa madai kuwa ana virusi.

•Pia aliweka wazi kwamba hana virusi vya UKIMWI kama ilivyodaiwa.

Diva na mumewe Abdul
Diva na mumewe Abdul
Image: INSTAGRAM// DIVA THE BAWSE

Mtangazaji wa Wasafi Media, Diva The Bawse amekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa watu ambao wamekuwa juu ya ndoa yake.

Siku ya Jumanne, Diva alilazimika kuanika matokeo ya vipimo vyake vya UKIMWI baada ya kuwepo kwa madai kuwa ana virusi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mtangazaji huyo mashuhuri alionyesha matokeo kutoka Hospitali ya TMJ yakibainisha wazi kuwa hana virusi. Alifichua kwamba alichukua vipimo vya ugonjwa huo siku ya Jumamosi.

"HIV 1& II- Hakuna," barua ya daktari aliyochapisha ilisomeka.

Hapo awali, mtangazaji na mchekeshaji maarufu wa Bongo, Mwijaku aliibua madai kwamba Diva tayari alikuwa ametemwa na mume wake kufuatia shida nyingi kwenye ndoa yao ya chini ya mwaka mmoja.

Mwijaku alidai kuwa sababu moja ya sababu ya Bw Abdul Razack kuachana na mtangazaji huyo ni kwa kuwa ana virusi. Pia alidai Diva hana uwezo wa kupata mtoto, hiivyo mumewe kamfukuza kwa kutomzalia.

"Naskia ni dada yenu ni positive kipimo kikubwa. Mganga kakimbia maradhi na ugumba. Mungu tusitiri ugonjwa huu wa ukimwi," alisema.

Katika majibu yake kwa Mwijaku, Diva hata hivyo alitupilia mbali madai ya kuachwa na kusisitiza kuwa ndoa yao bado ipo imara.

Pia aliweka wazi kwamba hana virusi vya UKIMWI kama ilivyodaiwa.

"Lile jipya ati la ugumba nalo hivi karibuni nitawapa jibu. Mungu mkali nyieee," Diva alisema kupitia Instastori.

Diva ambaye ni mtangazaji wa kipindi cha Lavi Davi kwenye Wasafi FM alifunga pingu za maisha na mume wake Sheikh Abdulrazak Salum katika hoteli ya Hyatt Regency Hotel, Dar es Salaam mwezi Machi mwaka jana.

Bosi wake Diamond Platnumz ni miongoni mwa wageni waalikwa wachache ambao walihudhuria hafla hiyo ya kufana.

Diamond alipokuwa akitoa hotuba yake alimpongeza mfanyikazi huyo wake kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akifanya Wasafi.

"Kiukweli, toka ulipokuja Wasafi Media, haujawahi kutuangusha. Shughuli unayoifanya pale, ni kipindi uko peke yako lakini unaifanya ikae ni kama mko watu ishirini.Unaifanya bora, kila mtu lazima akisikilize. Sio kazi rahisi, ni kazi kubwa, inahitaji mtangazaji ambaye ana akili, ana talanta ya kweli lakini pia anatumia muda kukaa nyumbani na kufikiria vitu anavyovifanya," Diamond alisema.

Kutokana na kazi yake  nzuri, Diamond aliahidi kumwongeza mtangazaji huyo mshahara kwa asilimia hamsini.

Pia aliahidi kumpatia Diva the Bawse runinga mpya, simu mbili mpya  na ugavi wa kila mwezi wa vinywaji vya soda.

Isitoshe, Diamond alimuagiza msaidizi wake Don Fumbwe kupatia wanandoa hao kipande chake cha ardhi kilicho karibu na bahari katika eneo la Kigamboni.

"Na millioni kumi kesho uwawekee kwenye akaunti," Diamond alisema.