Mwanamuziki Ringtone Apoko afichua jinsi anavyojipatia riziki

Apoko amedai kwamba anajipatia riziki kwa kumkasirisha shetani.

Muhtasari

•Ringtone ni miongoni mwa wasanii wa Kenya wanaoaminika kuwa matajiri wakubwa zaidi na wenye mali ya thamani.

•Ringtone zaidi alifichua kwamba mwaka huu mpya ameazimia kumuudhi shetani na wale wote wanaojihusisha naye.

Ringtone azungumzia utajiri wake.
Ringtone azungumzia utajiri wake.
Image: INSTAGRAM

Mwenyekiti wa kujitangaza wa Muungano wa Wasanii wa Injili nchini Kenya Alex 'Ringtone' Apoko amedai kwamba anajipatia riziki kwa kumkasirisha shetani.

Katika video ambayo alichapisha kwenye Instagram, mwimbaji huyo Injili pia aliweka wazi kwamba anajinufainisha kwa kuwakera wanaojihusisha na Shetani.

"Kuna watu wanauliza kazi yangu ni gani. Kazi yangu ni kukasirisha Shetani, Kazi yangu ni kukasirisha watu wa shetani, Kazi yangu ni kukasirisha wale wanaompenda shetani, Kazi yangu kukasirisha wale wanaomtetea shetani," alisema.

Ringtone zaidi alifichua kwamba mwaka huu mpya ameazimia kumuudhi shetani na wale wote wanaojihusisha naye.

Bila shaka, mwanamuziki huyo ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa zaidi nchini Kenya. Anaishi katika jumba la kifahari katika mtaa wa kifahari wa Runda, anaendesha gari kubwa na amekuwa akijigamba kuwa na nguo na mapambo ya bei ghali.

Kwa miaka mingi utajiri wa msanii huyo wa zamani wa nyimbo za injili umekuwa ukitiliwa shaka huku simulizi nyingi zikitolewa.

Mwaka jana mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa muziki wake ndio umefanikisha utajiri mkubwa ambao amejizolea kufikia sasa.

"Saa hii nimefikia bilioni. Mimi ni bilionea wa Kenya. Nilipata baada ya kuimba nyimbo za Mungu na nikatumia jina lake," alisema katika mahojiano.

Msanii huyo hata hivyo alibainisha kuwa mtu anahitaji "kutumia akili" ili aweze kuvuna vizuri kutoka kwa tasnia ya injili kama yeye.

"Kwa Mungu hufai kuenda ukisema asante pekee yake. Ukitaka chakula unafaa kuambia Mungu mara moja 'nataka chakula, nataka nyama, nataka kuku', lazima utoe maelezo, Mungu hupenda hivyo,"  Alisema.

Alijigamba kuwa utajiri wake mkubwa unatosha kuwafadhili wanamuziki wote wa muziki wa kutumbuiza wa Kenya.

"Mimi niko na pesa nyingi. Hata ninaweza kuifadhili tasnia ya muziki wa kidunia ya Kenya. Naweza kuwafadhili wote Siendi (kwa tasnia ya muziki wa kidunia) juu ya pesa," Ringtone alijibu kuhusu madai kwamba aligura injili ili kuwinda pesa.

Ringtone ni miongoni mwa wasanii wa Kenya wanaoaminika kuwa matajiri wakubwa zaidi na wenye mali ya thamani.

Kwa miaka mingi amekuwa akijiamba kuhusu utajiri wake huku akijiweka katika kiwango kimoja sawa na staa wa Bongo Diamond Platnumz