Mwanamuziki Trio Mio azungumza kuhusu matokeo yake ya KCSE

Trio Mio alionekana kujiamini alipokuwa akijibu kuhusu matarajio yake ya matokeo.

Muhtasari

• Trio Mio ni miongoni mwa watahiniwa zaidi ya 800,000 ambao walifanya mtihani wa mwaka jana wa kidato cha nne.

•Trio Mio ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote alisema, "zikam vile zinakam, sikosi usingizi mimi😂,"

Image: INSTAGRAM// TRIO MIO

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu anatarajiwa kutangaza matokeo ya mtihani wa KCSE 2022 ambao ulikamilika mwezi uliopita hivi karibuni.

Mwanamuziki mashuhuri wa kizazi kipya TJ Mario Kasela almaarufu Trio Mio ni miongoni mwa watahiniwa zaidi ya 800,000 ambao walifanya mtihani wa mwaka jana wa kidato cha nne.

Chini ya moja ya machapisho yake ya Instagram, shabiki mmoja alimuuliza kuhusu hisia zake kuelekea kutangazwa kwa matokeo.

"Trio results zinatoka hii wiki😂😂🔥.. Hata hivyo, upendo kwa wingi😍❤🔥," @it's nyambura.2 alimwambia.

Trio Mio ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote alisema, "zikam vile zinakam, sikosi usingizi mimi😂,"

Ina maana: (Yakuje vile yanakuja, sikosi usingizi mimi)

Mwezi Aprili mwaka jana, msanii huyo mwenye umri wa miaka 18 alitupitlia mbali madai kuwa alikalia mtihani wa KCSE 2021 na kupata alama D.

Trio Mio aliweka wazi kwamba hakuwahi kufanya mtihani huo wa kidato cha nne na kusema bado hakuwa amekamilisha masomo yake ya shule ya upili.

"Ni uwongo. Ni uwongo jo. Bado nasoma," Trio Mio alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Alilazimika kutoa ufafanuzi kufuatia tetesi kuwa alipata jumla ya alama D na kuandikisha alama E katika Hisabati na Kemia.

Hata hivyo alibainisha kwamba alikuwa mwanafunzi katika shule moja ya upili ya bweni nchini Kenya.

"Mimi nitaenda shule bado. Sisomei nyumbani. Mimi bado ni mwanafunzi wa bweni. Nitafika huko baadae,"  alisema.

Katika mahojiano ya mapema mwaka jana, mwanamuziki huyo alifichua kuwa angekalia mtihani wake wa KCSE mwishoni wa mwaka huo.

Trio alisisitiza kuwa usanii wake haungeaathiri masomo yake na kusema kila mara anapokuwa darasani alikuwa akiangazia masomo pekee.

"Kushughulikia muziki na masomo ni rahisi. Kila wakati mistari ikija huwa naandika vizuri, lakini haijawahi kuja mwalimu akiwa darasani. Hicho ndicho kitu cha maana kunitendekea. Haijawahi kutokea eti nianze kufikiria mambo na muziki mwalimu akiwa darasani" Mio alisema.