Mwanaume au mwanamke? Kinuthia hatimaye afichua jinsia yake halisi

Muhtasari

•Kelvin Kinuthia alisema kucheza uhusika wa kike kwenye video zake ni kwa ajili ya burudani na kazi tu.

•Kinuthia pia alithibitisha kuwa ana umri wa miaka  21 kwani wengi wamekuwa wakilitilia shaka jambo hilo.

Kelvin Kinuthia
Image: Mercy Mumo

Mburudishaji maarufu wa Tiktok Kelvin Kinuthia ameweka wazi kuwa yeye ni mwanaume.

Akiwa kwenye mahojiano, Kinuthia alisema kucheza uhusika wa kike kwenye video zake ni kwa ajili ya burudani na kazi tu.

Kinuthia alibainisha kuwa kamwe hajawahi kukana jinsia yake ya kiume. Hata hivyo aliweka wazi kuwa hayupo tayari kuacha kuigiza kama mwanamke kwa kuwa hiyo ndiyo riziki yake.

"Mimi ni mwanaume. Lakini nilisema siwezi wacha kufanya vitu nafanya kwa sababu watu wameniingililia ati nafanya vile na mimi ni mwanaume. Hiyo ndiyo imenifikisha mahali nipo," Kinuthia alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Mwanatiktok huyo alisema amekuwa akikejeliwa sana mitandaoni kwa kuigiza kama mwanamke ilhali yeye ni mwanaume.

Hata hivyo alidai kuwa nafasi hiyo ya kike ambayo anacheza imefanya apate kazi za kufanya matangazo ya mavazi na mapambo ya kike.

"Hakuna vile nitaanza kubadilisha mhusika. Hata watu wataboeka. Kuna watu tayari wamezoea jinsi Kinuthia alivyo. Hakuna mahali ambapo nimewahi kusema kuwa mimi sio mwanaume. Ni kazi na hiyo ndiyo imenifikisha mahali nilipo," Alisema.

Kinuthia alizua gumzo mitandaoni baada ya kupakia picha ya kitambulisho chake kwenye Instagram siku chache zilizopita.

Mwanatiktok huyo alitaka kuthibitisha kuwa ana umri wa miaka  21 kwani wengi wamekuwa wakilitilia shaka jambo hilo.

"Watu wa kwani ulizaliwa 2001 ndio hii sasa mkikosa kuamini shida yenu sasa. Na birthday ni mwezi ujao," Kinuthia aliandika juu ya picha ya kitambulisho chake.

Licha ya kuwa lengo lake lilikuwa kuthibitisha umri, wanamitandao wengi waliangazia macho kwenye jinsia iliyokuwa imenakiliwa pale. 

Kitambulisho cha Kinuthia kilithibitisha kuwa yeye ni mwanaume na wanamitandao wakazua mdahalo mkali kufuatia hayo.