“Mzungu karibu anitoe roho, kilinichoma!” Akothee ajutia ndoa yake na ‘Omosh’

Akothee alijigamba kuhusu mapenzi ya Nelly Oaks kwake na kukejeli ndoa yake iliyovunjika na Denis ‘Omosh’ Schweizer.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alisikika akimuita Nelly Oaks ‘bae’ mara kadhaa, jina ambalo hutumika sana na wapenzi.

•Akothee alizungumzia masaibu yake na aliyekuwa mumewe akisema, “Mzungu karibu anitoe roho, nitakuja kuwaelezea siku moja.”

Mwimbaji Akothee na mpenzi wake Bw Schweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mfanyabiashara mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee hivi majuzi alishiriki katika kipindi cha moja kwa moja kwenye Tiktok na meneja wake Nelly Oaks.

Katika kipindi hicho cha moja kwa moja, Nelly Oaks alionekana jikoni akimuandalia chakula mwimbaji huyo ambaye alikuwa kwenye chumba cha kupumzika akizungumza naye na mashabiki.

Meneja huyo alifichua kuwa alikuwa akimtayarishia Akothee chakula maalum kwa sababu maalum.

“Kwa kweli huwezi kuja jikoni. Hii ni chakula cha jioni maalum kwa mtu maalum kama wewe. Ni surprise,” Nelly Oaks alisikika akimwambia Akothee alipoomba kwenda kumsaidia jikoni.

Katika kipindi hicho, mama huyo wa watoto watano alisikika akimuita Nelly Oaks ‘bae’ mara kadhaa, jina ambalo hutumika sana na wapenzi.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alisikika akijigamba kuhusu mapenzi ya Nelly Oaks kwake na pia kukejeli ndoa yake iliyovunjika na Denis ‘Omosh’ Schweizer.

“Ni vizuri sana kupendwa, nilikuwa nimeenda huko (to Schweizer) nikifikiria ni , ati greener pastures, kimenichoma!!.. Ati mzungu wueh! Kumbe mzungu!,” Akothee alisema.

Aliendelea kuzungumzia masaibu yake na aliyekuwa mume wake mzungu akisema, “Mzungu karibu anitoe roho, nitakuja kuwaelezea siku moja.”

Katika kipindi hicho, Akothee pia aliwazima vikali wanawake waliokiri kuvutiwa na meneja huyo wake akisema kuwa tayari amempata na hayuko tayari kwao.

Mwimbaji huyo kwa kejeli aliwataka wanawake hao badala yake wamtafute aliyekuwa mumewe, Denis Schweizer akibainisha kuwa mzungu huyo kwa sasa hana mchumba.

“Kwa nini mnang’ang’ania na Nelly Oaks. Si muende mchukue Omosh, muende mchukue Omosh wa Pakistan. Yeye ndiye ako single,” alisema.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mama huyo wa watoto 5 kuthibitisha kugonga mwamba kwa ndoa yake na mzungu huyo kutoka Uswizi.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alithibitisha kuvunjika kwa ndoa yake na Denis Shweizer mwisho mwa mwezi Oktoba. Alithibitisha hayo alipokuwa akishiriki kipindi cha moja kwa moja na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kipindi hicho, alithibitisha kwamba aligura ndoa yake ya muda mfupi mnamo mwezi Juni wakati yeye na Omosh walipokuwa kwenye fungate.

“Nimehama kutoka kwa mahusiano hayo. Hayapo tena. Ninataka kuwaaambia kwamba nilitoka kwenye uhusiano huo mwezi Juni. Hata hivyo sitaeleza kwa undani,” Akothee alisema.

Aliongeza, “Nilifurahia ndoa yangu, nilifurahia harusi yangu. Sijutii chochote. Nilifanya harusi yangu mnamo siku ya kuzaliwa kwangu ndio ikiwa tu mambo yangeenda vibaya, kama wamefanya, basi singekuwa na majuto yoyote.”