Nabayet ajibu kuhusu kurudiana na Otile Brown baada ya kukutana Ethiopia

Otile Brown kwa sasa yuko jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Muhtasari

•Inadaiwa kwamba Otile Brown alizuru Ethiopia ili kumuona mpenzi wake wa zamani Nabayet almaarufu Nabbi.

•Wanamitandao mehitimisha kuwa wawili hao walikutana na sasa wanawasihi wafufue mahusiano yao. 

Otile Brown na Nabayet katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Mwimbaji mashuhuri wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown kwa sasa yuko jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Tetesi zinazosambaa mjini kwa sasa ni kwamba mwanamuziki huyo mahiri mwenye umri wa miaka 30 alizuru taifa hilo la Afrika Kaskazini ili kumuona mpenzi wake wa zamani Nabayet almaarufu Nabbi.

Otile alifanya safari hiyo mapema wiki hii lakini hakufichua madhumuni ya ziara yake.

Siku ya Jumanne, alichapisha picha yake akiwa amesimama nje ya nyumba moja katika mji mkuu wa Ethiopia. Pichani alikuwa amevalia shati nyeupe, t-shati nyeusi, suruali nyeusi na kiatu cheupe huku akiwa amebeba mkoba.

"Soma maisha...," aliandika chini ya picha hiyo ambayo alipakia Instagram.

Nabayet, ambaye ni mzaliwa wa Ethiopia, pia alichapisha picha kwenye Instastori zake ambayo ilimuonyesha akiwa katika hoteli moja jijini Addis Ababa.

Kwenye picha, mkono wa mwanaume uliokuwa na pete kwenye kidole cha pete ulionekana. Pia, mwanamume huyo alikuwa amevalia shati jeupe na wanamitandao wamefanikiwa kumtambua kuwa sio mwingine bali ni Otile Brown.

Wakenya watumizi wa Instagram wamehitimisha kuwa wapenzi hao wa zamani walikutana na sasa wanawasihi wafufue mahusiano yao. Baadhi ya mashabiki wao wametumia sehemu za maoni kwenye machapisho yao kuwaomba warudiane.

@domy.cruz Rudi tu na Nabayet

@njengageorge150 Ukuje na nabayet bro.. usikuje pekee yako😂

@2923nas Chini kwa goti lako na umchumbie sasa

Nabayet hata aliendelea zaidi kuwajibu baadhi ya wanamitandao waliomuomba aandamane na mwimbaji huyo kurudi Kenya.

"Nabbi anza kufunga virago tayari 😍 unapanda ndege ya kwanza 🛫 kwenda Kenya asubuhi 🌄," @iam_anitarita alimwambia.

Alijibu, "❤❤."

@kendwaelinahm alimwambia, " TunakupendaNabbi ❤️🇰🇪 " akajibu "🇰🇪❤."

Mwimbaji Otile Brown alithibitisha kutengana kwake na Nabbi mnamo wezi Januari mwaka jana baada ya kuchumbiana naye kwa karibu miaka mitatu. Wawili hao walijitosa kwenye mahusiano mapema mwaka wa 2019, miezi michache tu baada ya Otile kutengana na mwanasoshalaiti maarufu Vera Sidika.

Wakati akitangaza kutengana kwao kupitia ukurasa wake wa Instagram, Otile alifichua kuwa mara ya mwisho alipokutana na Nabbi alitaka kujua jinsi wangeendelea na wakakubaliana kwenda tofauti.

"Mimi na Nabbi hatuko pamoja tena… Mara ya mwisho tulikuwa pamoja ilikuwa kujaribu kutafuta njia ya kusonga mbele lakini tuliamua kwenda tofauti kwa bahati mbaya," Mwanamuziki huyo alisema.