"Najihisi mwanaume kamili!" Harmonize ajivunia furaha kurejea katika familia yake na Kajala

Harmonize amesema ilikuwa ndoto yake kuona familia yake ikiwa na furaha pamoja.

Muhtasari

•Harmonize ameeleza furaha yake kuona familia yake mpya ikiwa na furaha pamoja na kufichua kuwa ilikuwa ndoto yake siku zote.

•Harmonize amesema furaha ya familia yake iliyoonekana katika video hiyo inamfanya ajisikie mwanaume kamili.

Harmonize, Kajala Masanja na Paula Kajala
Image: INSTAGRAM//

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameonekana kuridhishwa na uhusiano wa sasa kati ya mchumba wake Kajala Masanja na bintiye Paula.

Bosi huyo wa Kondegang ameeleza furaha yake kuona familia yake mpya ikiwa na furaha pamoja na kufichua kuwa ilikuwa ndoto yake siku zote.

"Wooo!!, ilikuwa ndoto kuona familia yangu ikiwa na furaha tena na Mungu alifanya hivi," alisema kwenye Instastori zake.

Konde Boy alikuwa akijibu video ya Tiktok iliyowaonyesha Kajala na Paula wakicheza densi pamoja. Katika video hiyo, mama huyo na bintiye walionekana wenye furaha kwenye walipokuwa wakicheza pamoja.

Harmonize amesema furaha ya familia yake iliyoonekana katika video hiyo inamfanya ajisikie mwanaume kamili.

"Kila alichopanga Mungu kitatokea!! Usikatishwe tamaa, usikate tamaa!!," aliandika.

Amani, upendo na furaha zinaonekana kurejea tena nyumbani kwa Harmonize katika siku za hivi majuzi. 

Matukio kadhaa ya siku za hivi majuzi yameashiria kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Harmonize , mchumba wake na bintiye wa kambo.

Mapema mwezi huu, Paula alionyesha wazi kujivunia kwake katika mahusiano ya mama yake na Harmonize. Mwanamitindo huyo aliwasifia wachumba hao baada ya yao kupakia klipu iliyoonyesha wakicheza ngoma zao mpya  'Amelowa' na 'Nitaubeba'.

Harmonize pia amejivunia binti huyo wake wa kambo mara kadhaa hapo awali. Siku kadhaa zilizopita alimsifia mwanamitindo huyo huku akisema anamuonea fahari kama tajiri mdogo baada ya kufungua duka lake la kuuza nguo.

“Yaani nakuonea Fahari sana @therealpaulahkajala, Tajiri mdogo Oyaaa. Nani anaweza kufanya Bora kuliko Binti yangu,” alisema.

Uhusiano kati ya Harmonize na Kajala umeendelea kunoga kadri siku zinavyosonga tangu kurudiana kwao miezi kadhaa iliyopita.

Wawili hao walikuwa wametengana Aprili mwaka jana kufuatia madai kuwa staa huyo wa Bongo alikuwa akimtongoza Paula.

Kwa kipindi kirefu Paula na Harmonize walikuwa hawaelewani na inaaminika kuwa madai hayo huenda yalichangia.

Ingawa Paula ameonekana kumkubali Harmonize kama babake, baba yake mzazi ni mtayarishaji maarufu P-Funk Majani.