"Nataka kuwa single milele!" Harmonize amjibu mwanadada aliyechora tattoo ya uso wake, afichua kwa nini

Konde Boy alidokeza kwamba katika mahusiano yake ya awali alidanganywa sana.

Muhtasari

•Bosi huyo wa Kondegang alionyesha video ya tattoo ya mwanadada huyo na kupongeza upendo wa baadhi ya watu kwake.

•Wakati huo huo, mwimbaji huyo alidokeza kwamba alijitoa mali na hali ili kumridhisha mpenzi wake wa zamani.

Mwimbaji wa Bongo, Harmonize
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amemthamini mwanadada mmoja ambaye alichora tattoo ya uso wake kwenye ngozi yake.

Siku ya  Jumanne jioni, bosi huyo wa Kondegang alionyesha video ya tattoo ya mwanadada huyo na kupongeza upendo wa baadhi ya watu kwake.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba hayupo tayari kujaribu mahusiano mapya baada ya kuvunjwa moyo mwishoni mwa mwaka jana.

"Asante kwa hili mpendwa, Mungu akubariki mtoto wa kike. Lakini, niko single!" alisema kwenye video hiyo aliyochapisha Instagram.

Konde Boy alidokeza kwamba ni vigumu kwake kujitosa kwenye mahusiano mengine kwa kuwa imekuwa vigumu kwake kumwamini yeyote.

Aidha, alidokeza kwamba wakati akiwa kwenye mahusiano yake ya awali alidanganywa sana na wapenzi ambao hakuwafichua.

"Kuna wasichana ambao wananipenda kabisa. Ni vigumu sana kwangu kumwamini mtu yeyote TENA!!! Ewe Mungu, NATAKA KUWA SINGLE MILELE . Siwezi kukubali uongo tena," Alisema staa huyo wa Bongo.

Wakati huo huo, mwimbaji huyo alidokeza kwamba alijitoa mali na hali ili kumridhisha mpenzi wake wa zamani.

Kufuatia hilo, hasidi huyo wa Diamond Platnumz amewashauri wanaume kuzingatia kutengeneza pesa badala ya mapenzi.

Wiki iliyopita, Konde Boy  alithibitisha kuwa hayupo kwenye mahusiano yoyote kwa sasa.

Katika taarifa yake, alisema kwa sasa anajipatia muda usiojulikana wa mapumziko kabla ya kujitosa kwenye mahusiano mapya.

"Msijali, hivi karibuni nitapata mtu na mtamjua!!," alisema.

Staa huyo wa Bongo alidokeza kwamba alipitia masaibu mengi mno wakati akiwa katika mahusiano yake ya awali.

Alionekana kuwakashifu wakosoaji na kuwataka wasite kumhukumu kwa kuwa hawana ufahamu wowote wa aliyopitia.

"Wasikuone na kidem tuu!! Hivi mnajua niliyo yapitia," aliandika.

Aliyekuwa mpenzi wake wa hivi majuzi, muigizaji  Frida Kajala Masanja alithibitisha kuvunjika kwa mahusiano yao mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuchumbiana naye kwa takriban miezi saba.