"Ni miezi 5 tangu nimwone!" Mulamwah afichua sababu za kutokuwa katika maisha ya bintiye

Muhtasari

•Mulamwah alisema uhusiano mbaya wa sasa kati yake na mzazi mwenzake umefanya ushirikiano katika malezi kuwa mgumu.

•Mulamwah hata hivyo alifichua kwamba kila mwezi huwa anaweka shilingi laki moja kwenye akaunti ya bintiye ambayo atamkabidhi wakati siku za usoni.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amekiri kuwa miezi mitano imepita tangu mara yake ya mwisho kumwona binti yake.

Akishirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu (Q&A) kwenye Instagram, Mulamwah alisema uhusiano mbaya wa sasa kati yake na mzazi mwenzake umefanya ushirikiano katika malezi kuwa mgumu.

Mulamwah alidai kwamba familia yake haijawahi kupata nafasi ya kukutana na mtoto wake ambaye atatimiza miezi saba mwezi huu. 

"Nimeblockiwa kila mahali, wazazi wetu wamekasirikiana, mambo yameharibika. Familia yangu haijawahi kukutana na mtoto huyo tangu kuzaliwa kwake isipokuwa baba yangu ambaye alifunga safari kutoka Kitale kuja Nairobi. Tulikuwa tumepangia binti yangu karamu nyumbani, kila mtu alihudhuria lakini hakuja na K," Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni muuguzi alidai hajawahi kupata nafasi ya kuwepo katika maisha ya binti yake.

Mulamwah hata hivyo alifichua kwamba kila mwezi huwa anaweka shilingi laki moja kwenye akaunti ya bintiye ambayo atamkabidhi wakati siku za usoni.

"Najua atapata miguu na atakuja kunitafuta siku moja. Kazi yangu ni kuwa tayari wakati huo ukifika," Alisema.

Carol Muthoni alipotembelea studio zetu takriban mwezi mmoja uliopita alidai mara ya mwisho kwa Mulamwah kumuona mtoto wao ni akiwa na umri wa miezi miwili tu.

Mwigizaji huyo alisema hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi huyo wake wa zamani na kumwomba apige hatua ya kuenda kumwona binti yao.

"Tenga wakati uje uone mtoto wako, anaendelea vizuri. Ningependa uje uwe katika maisha yake. Uko karibu kila wakati. Hatukukatazi kuja kuona mtoto. Unajua kwangu ni kwako pia. Usijihisi umetengwa," Muthoni alisema.