"Ni usaliti mkubwa zaidi kuwahi kutokea!" Jalang'o azungumzia kuwarejesha kazini wafanyikazi waliomwibia

Muhtasari

•Jalang'o alisema wafanyikazi hao wake kwa muda mrefu walitoweka na familia zao punde baada ya kuiba pesa zile.

•Alisema ingawa yupo tayari kuwasamehe wawili hao, nafasi ya kufanya kazi nao tena ni nadra sana.

Mchekeshaji Jalang'o akiwa na wafanyakazi wake wawili waliomwibia
Mchekeshaji Jalang'o akiwa na wafanyakazi wake wawili waliomwibia
Image: HISANI

Mgombea ubunge wa Lang'ata Felix Odiwour almaarufu Jalang'o ameweka wazi kuwa kuibiwa pesa na wafanyikazi wake ndio usaliti mkubwa zaidi amewahi kukumbana nao.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Jalang'o alisisitiza kuwa ni kweli Morrison Litiema na Eli Khumundu waliiba kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa gari ya mkewe.

Mtangazaji huyo wa zamani alisema wafanyikazi hao wake kwa muda mrefu walitoweka na familia zao punde baada ya kuiba pesa zile.

"Walichukua nguo na wakaenda. Tulijaribu kuwatafuta, walikuwa wamezima simu, DCI walikuwa na njia za kuwafuatilia. Tuliambiwa wapo njiani kuelekea Bungoma," Alisema.

Alifichua kuwa wawili hao wao walipiga hatua ya kuwasiliana naye siku kadhaa zilizopita. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na walichozungumza kuhusu.

"Ni kesi ambayo iko mikononi mwa polisi lakini ndio usaliti mkubwa zaidi ambao nimewahi kukumbana nao maishani. Natumai haitabadilisha jinsi ambavyo huwa nachukulia watu," Alisema.

Jalang'o ambaye atazamia kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu alisema hakuwahi kufikiria wafanyikazi hao wake wangewahi kuiba kutoka kwake.

Alisema ingawa yupo tayari kuwasamehe wawili hao, nafasi ya kufanya kazi nao tena ni nadra sana.

"Nitawasamehe lakini sidhani nitawahi kuwa nao kazini tena. Nilizungumza na marafiki kadhaa, mimi nilikuwa tayari lakini nikizungumza na watu nimegundua kuwa huu ndio usaliti mkubwa kuwahi kutokea," Alisema.

Mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa tayari kuna wafanyikazi wengine ambao wamechukua kazi ambazo Eli na Litiema walifanya.

Alisema wafanyikazi hao wake walifanya kosa kubwa na kudai itakuwa ngumu kwao kuwahi kupata kazi kwingine.

"Watu wanawajua. Hakuna mtu ambaye atawaajiri. Kuna ujinga ingine ambapo unajiharibia vitu vingi maishani,"