"Niko tayari kufa hapa!" Akothee ajivunia mahusiano yake mapya

Mwimbaji huyo amesema tangu alipokutana na Bw Schweizer amejua jinsi inavyohisiwa kupendwa.

Muhtasari

•Akothee ametangaza kuwa hayupo sokoni tena na tayari ametulia katika mahusiano yake mapya.

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 alikiri kuwa hapo awali hakuwahi kujua kuna penzi la kweli.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Akothee anaonekana mwenye furaha na kuridhika katika mahusiano yake mapya na mpenzi wake wa kizungu.

Takriban mwezi mmoja umepita sasa tangu mama huyo wa watoto watano amfichue mpenziwe mpya baada ya kutengana na Nelly Oaks.

Sasa kupitia ukurasa wake wa Instagram ametangaza kuwa hayupo sokoni tena na tayari ametulia katika mahusiano yake mapya.

"Anaposema wewe ni mke wangu na maisha yangu 🙈 mwenzenu sina nguv . Akothee hayupo sokoni, amechukuliwa, ametulia na anastarehe," aliandika chini ya picha inayoonyesha akitabasamu kitandani.

Katika chapisho lingine msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 alikiri kuwa hapo awali hakuwahi kujua kuna penzi la kweli.

Alisema tangu alipokutana na mpenzi wake mpya Bw Schweizer sasa amejua jinsi inavyohisiwa kupendwa.

"Mpenzi, sikuwahi kujua kuna mapenzi ya kweli, siku zote niliogopa kudhulumiwa. Hadi nilipokutana na wewe mpenzi, ikiwa ndivyo mtu anavyohisi kupendwa, basi niko tayari kufa hapa, ona niking'aa," alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakejeli wakosoaji ambao wanadai kuwa gari alilonunuliwa na mpenzi wake ni mali ya kaunti.

Akothee aliyaweka wazi mahusiano yake mapya mapema mwezi uliopita. Wiki chache zilizopita alidokeza kufunga pingu za maisha na mzungu huyo.

Alisema kwa sasa anachumbiana na mwanaume huyo pekee na kubainisha kuwa hayupo kwenye mahusiano mengine ya kando.

Pia alionekana kujivunia kuwa sasa amepata mzungu mdogo , tofauti na wazungu wazee aliowahi kuwa nao hapo awali.

"Wee kama angekua guka ,zile matusi ningepokea , ni Mungu tuu. Mungu wa Akothee akupate pia .Nakupenda mpenzi❤," alisema katika chapisho lingine.

Aliongeza, "Ninachumbiana na mwanaume mmoja kwa wakati mmoja, nina moyo mmoja tu, nikifa nakufa. Niko bize kupenda huyu hakuna wakati kwa mtu mwingine yeyote. Hiyo ndiyo tofauti kati yangu na wewe."

Mama huyo wa watoto watano alitangaza kutengana kwake na aliyekuwa mpenziwe kwa muda mrefu, Nelly Oaks mapema mwaka huu.