"Nilipata amani badala ya kulipiza kisasi" Kajala azungumzia mahusiano yake na Harmonize yaliyosambaratika

"Mimi ni mbaya kuliko mabaya ambayo watu hawa wananitakia," Kajala alisema

Muhtasari

•Kajala amekuwa jijini Dubai ambako amekuwa akitumia wakati mzuri na binti yake wa miaka 20 Paula Paul.

•Katika chapisho lingine,  muigizaji huyo alionekana kuzungumzia mahusiano yake wa muda mfupi na Harmonize.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Muigizaji wa filamu Bongo Fridah Kajala Masanja ameendelea kufurahia maisha yake hata baada ya kutengana na bosi wa Konde Music Worldwide, Rajab Kahali almaarufu Harmonize takriban miezi miwili iliyopita.

Kajala amekuwa jijini Dubai ambako amekuwa akitumia wakati mzuri na binti yake wa miaka 20 Paula Paul. Hivi majuzi wawili hao wamekuwa wakionyesha picha za kumbukumbu nzuri walizotengeza huko.

Mchumba huyo wa zamani wa Harmonize pia amekuwa akitumia machapisho yake kutuma jumbe fiche kuhusu maisha yake.

"Mimi ni mbaya kuliko mabaya ambayo watu hawa wananitakia," alisema katika chapisho lake moja la hivi majuzi.

Katika chapisho lingine,  muigizaji huyo alionekana kuzungumzia mahusiano yake wa muda mfupi na Harmonize.

Kajala alionekana kutupilia mbali madai kwamba alirudiana na staa huyo wa Bongo ili kulipiza kisasi kwa maovu aliyomtendea yeye na familia yake hapo awali na kusambaratisha mahusiano yao mwezi Aprili 2021.

"Mwanamke aliyepata amani badala ya kulipiza kisasi kamwe hawezi kusumbuliwa," alisema kwenye picha inayomuonyesha akipata mlo na kinywaji jijini Dubai ambayo alichapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Muigizaji huyo alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake ya miezi kadhaa na Harmonize mapema mwezi Desemba.

Ingawa hakuweka wazi kilichowatenganisha, alibainisha kuwa hakubeba kinyongo dhidi ya mwimbaji huyo licha ya mahusiano kugonga mwamba.

Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.

Mama huyo wa binti mmoja aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano kusambaratika.

Wawili hao walikuwa wamerudiana mapema mwaka jana baada ya kuwa wametengana kwa takriban mwaka mmoja.

Mahusiano yao ya kwanza yaliisha Aprili 2021 huku Harmonize akidaiwa kujaribu kumtongoza bintiye Kajala, Paula.