Nilipokea vitisho vya kifo kwa kupiga picha na Raila- Mwanadada asimulia

Muhtasari

•Mbote alisema hakujua kupiga picha na waziri huyo mkuu wa zamani kungehatarisha maisha yake.

•Anasema mfanyibiashara Jimmy Wanjigi alikuwa na Raila wakati huo na ndiye alimwomba atoe simu yake ili picha hizo zipigwe.

•Anasema ni kujali na faraja ya wazazi wake ambayo ilimwezesha kuvuka nyakati za msukosuko zilizosababishwa na majibu ya picha hiyo.

Raila Odinga na Sasha Mbote
Raila Odinga na Sasha Mbote
Image: HISANI

Sasha Mbote, mwtaalamu wa masaji alionekana kwenye picha na kinara wa ODM Raila Odinga mwaka wa 2019, anasema maisha yake hayakuwa sawa baada ya picha hiyo kusambaa mitandaoni.

Katika mahojiano na Lynn Ngugi, Mbote alisema hakujua kupiga picha na waziri huyo mkuu wa zamani kungehatarisha maisha yake.

 “Ilikuwa siku ya kawaida kwangu, jioni nilienda hoteli fulani kunywa chupa chache za bia, nilitamani kupata chakula cha jioni lakini niliangalia saa nikaona ni usiku sana, nikamuita mhudumu na kumuomba aangalie meza yangu ili niweze kukimbia msalani," alisema.

Mbote anasema alipokuwa anaelekea msalani aliona meza iliyokuwa na wanaume watano na mmoja wao alikuwa Raila.

Kama shabiki yeyote wa Raila, Mbote aliomba picha.

"Nilikuwa kama oh Mungu wangu, Baba. Nilimuona tu kama mtu anayenijua. Alisema sasa na mimi nikaelekea msalani. Niliporudi, nilimuuliza kama ningeweza kupiga naye picha," alisema.

"Nilitaka kuwathibitishia wazazi wangu kwamba nimekutana na Raila. Hawangeamini nilikutana naye bila picha."

Anasema mfanyibiashara Jimmy Wanjigi alikuwa na Raila wakati huo na ndiye alimwomba atoe simu yake ili picha hizo zipigwe.

Mbote anasema baada ya Wanjigi kupiga picha hizo, alizisambaza mtandaoni bila kujua aina ya hisia ambazo ziketolewa.

Kulingana naye, baadhi ya watu waliona picha hiyo walidhani kwamba alikuwa mpango wa kando wa Raila huku wengine wakidhani anatumiwa na vyama pinzani vya kisiasa kumwangamiza Baba.

"Nilipowasha simu yangu, meseji hazikuacha kuingia, watu walikuwa wakiniita kila aina ya majina, walisema nimelipwa ili kumuua Baba."

Alifichua kuwa ni kujali na faraja ya wazazi wake ambayo ilimwezesha kuvuka nyakati za msukosuko zilizosababishwa na majibu ya picha hiyo.

"Ikiwa wazazi wangu wangetilia shaka utu wangu, ningejitoa uhai."

(Utafsiri: Samuel Maina)