"Nimechekwa vya kutosha!" Ukubwa wa pua la mwandani wa Diamond, Baba Levo kupunguzwa

Muhtasari

•Haya yanajiri baada ya msanii huyo kukejeliwa sana hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na ukubwa wa pua lake.

•Mwanamuziki huyo pia ametangaza kuwa anapanga kufanyiwa upasuaji wa kupunguza kitambi chake.

Image: INSTAGRAM// BABA LEVO

Mwanamuziki wa Bongo Revokatus Kipando almaarufu Baba Levo amefichua kuwa anapanga kufanyiwa upasuaji wa pua.

Haya yanajiri baada ya msanii huyo kukejeliwa sana hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na ukubwa wa pua lake.

Baba Levo ameweka wazi kuwa anapanga kuenda nchini Uturuki ili pua lake lipunguzwe hadi ukubwa wa kawaida.

"Nimepanga kuenda Uturuki kwa ajili ya kuhakikisha  nafanya upasuaji. Nimechekwa vya kutosha. Muda umefika niende nikafanyiwe upasuaji, nikatwe pua liwe ndogo la kawaida na kila kitu kiwe sawa," Baba Levo alisema.

Mwanamuziki huyo pia ametangaza kuwa anapanga kufanyiwa upasuaji wa kupunguza kitambi chake.

Amefichua kuwa huduma zote za upasuaji zinakadiriwa kugharimu shilingi milioni 46 za Tanzania (Ksh 2.3M), zote ambazo msanii wake YJ ameahidi kugharamia.

"Mimi ndio nitasimamia hiyo shughuli, pia ndege. Vyote nitalipia. Kila kitu," YJ alisema.

Baba Levo amesisitiza kuwa hana hofu yoyote kuhusu madhara ya kufanyiwa upasuaji huo wa pua na kitambi.

Wanamitandao wengi wamekuwa wakimkejeli mwanadani huyo wa Diamond Platnumz kutokana na unene wa pua. 

Wengi wamekuwa wakiandika jumbe za kejeli chini ya picha ambazo msanii huyo hupakia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.