"Nimerudi kwa ufalme wa Mungu!" Ringtone Apoko afichua kwa nini alikuwa amegura injili

"Nimerudi kwa ufalme wa Mungu. Siwezi kubackslide!" Alisema.

Muhtasari

•Ringtone amedai kuwa alipandishwa cheo katika jeshi la Kristo na kutumwa kwenye misheni ya siri ili kuchunguza mipango ya shetani.

•Mwezi jana alidai kuwa alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa wanawake wengi walikuwa wakimuangazia .

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwimbaji wa nyimbo za injili Ringtone Apoko ametangaza kwamba amejea kwenye wokovu wiki chache tu baada ya kugura.

Kupitia kanda ya video ambayo alipakia kwenye Instagram, Ringtone aliweka wazi kwamba hakuwa amegura injili bali alikuwa kwenye misheni ya siri katika tasnia ya kidunia.

Mwimbaji huyo aliyezingirwa na utata mwingi katika taaluma yake ya miaka mingi amedai kuwa alipandishwa cheo katika jeshi la Kristo na kutumwa kwenye misheni ya siri ili kuchunguza mipango ya shetani.

"Mimi ni mkubwa sana katika cheo cha jeshi la Yesu. Hata shetani akiniona hawezi kuniamini. Shetani akiniona anafikiria nimetumwa na mafuta na kiberiti tukawachome huku Jehanamu. Mimi siwezi kubackslide. Nilikuwa nimeenda undercover mission ya kuweza kujua mambo ambayo shetani anapanga," Apoko alisema.

Alidai kuwa misheni yake ilizaa matunda na kutangaza kuwa matokeo yake yatasaidia kuangusha ufalme wa shetani.

"Nimerudi kwa ufalme wa Mungu. Siwezi kubackslide!" Alisema.

Mapema mwezi jana Ringtone alitangaza hatua yake ya kugura injili na kujiunga na tasnia ya muziki wa kimapenzi.

Mwimbaji huyo alidai kuwa wanawake ndio waliochangia zaidi uamuzi wake kugura injili. Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mashabiki wake wengi wa kike walikuwa wakimuangazia yeye badala ya kufuata injili aliyoimba.

"Naimba alafu wale wasichana ambao wananipenda wananifuata mimi badala wafuate Yesu. Nataka break kidogo. Nataka wasichana wamuangazie Yesu waachane na mimi," Ringtone alisema katika mahojiano na Mpasho.

Apoko ambaye amekuwa akiimba nyimbo za injili kwa zaidi ya mwongo mmoja alijigamba kuwa anamezewa mate na kundi kubwa la wanadada.

Aidha mwanamuziki huyo alipuuzilia mbali madai kuwa aligura injili kwa minajili ya mapato ya kifedha na kudai kuwa tayari amejizolea utajiri mkubwa kutokana na kazi yake ya muziki wa injili.

"Niko na pesa nyingi. Hata naweza nikafadhili sekta ya muziki wa kidunia ya Kenya. Naweza wafadhili wote. Siwezi kuenda huko kwa sababu ya pesa," Alisema.

Apoko alikuwa ameahidi kuachia wimbo wa mapenzi baada ya kuipa kisogo tasnia ya nyimbo za injili.

"Nimerudi kwa ufalme wa Mungu!" Ringtone afichua aliyoshuhudia baada ya kugura injili