"Ningeavya mimba yako, hakungekuwa na birthday" Akothee afoka baada ya kutoalikwa na bintiye

"Mko wapi? Msinifanyie hivi tafadhali! Mnachomfanyia mama yenu kitafanyiwa kwenu pia," Akothee alilalamika.

Muhtasari

•Akothee alilalamika kwa kejeli baada ya kutoalikwa kwenye karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye mzaliwa wa kwanza, Vesha Okello.

•Ili kuwaadhibu kwa kutomwalika kwenye sherehe, alifunga mlango na kiti na kuwaonya kuhusu kurudi nyumbani.

Akothee na mabinti zake
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Jumanne, mwanamuziki Akothee alilalamika kwa kejeli baada ya kutoalikwa kwenye karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye mzaliwa wa kwanza, Vesha Okello.

Kulingana na mama huyo wa watoto watano, mabinti zake Vesha na Okello walifanya karamu ya siku ya kuzaliwa katika eneo lisilojulikana lakini hawakumwalika.

Alifoka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akihoji waliko binti zake na kulalamika kuhusu ni kwa nini walikosa kumwalika.

"Hawa wasichana wanafanya karamu ya siku ya kuzaliwa mahali fulani na mimi sijaalikwa 🤔🤔🤔🤔 Mko wapi? Msinifanyie hivi tafadhali! Mnachomfanyia mama yenu kitafanyiwa kwenu pia 🤔🤔 Vesha Okello ikiwa ningeavya mimba yako, Kusingekuwa na karamu ya siku ya kuzaliwa, Rue.Baby,” Akothee alilalamika.

Akothee aliendelea kuomba yeyote ambaye angewaona wasichana hao vijana wakiburudika mahali fulani amjulishe.

Katika chapisho lingine, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alilalamika kuhusu wasichana hao wawili kutopokea simu zake ilhali alihitaji usaidizi wa kufungua mlango.

“Wewe mhudumu anaona watoto wangu hapo . Waambie watoto wangu Vesha Okello na Rue baby wanitunie code ya mlango nimesahau Nika block , hawachukui simu wanadhani nawasaka. Nimesimama nje kwa baridi nitageuka theluji,” alisema.

Baadaye alitoa sasisho nyingine mwendo wa usiku wa manane akisema kwamba wasichana hao walikuwa bado hawajarudi nyumbani. Ili kuwaadhibu kwa kutomwalika kwenye sherehe, alifunga mlango na kiti na kuwaonya kuhusu kurudi nyumbani.

“Msijaribu kurudi, nimelala. Watag ili wasome hisia," alisema.

Mapema Jumanne, Akothee alimsherehekea binti yake mzaliwa wa kwanza Vesha Okello kwa ujumbe mzuri akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika barua aliyomwandikia Vesha siku ya Jumanne, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alimtambua binti yake kwa majina mazuri na kumtaja kuwa mtoto mwenye nidhamu.

Akothee aliorodhesha baadhi ya mafanikio makubwa ambayo mtoto huyo wake wa kwanza amefanikiwa kupata  kufikia hadi sasa, mengi ambayo yeye mwenyewe hakuweza kufikia katika umri huo.

"Binti Mpendwa, Kwa malkia wa moyo wangu, rafiki yangu mkubwa na mlinzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Savy House, Bi Mkurugenzi wa Akothee Safaris, na mama wa wajukuu zangu...," Akothee alianza barua yake.

Aliendelea kuandika, “Wewe ni mtoto mwenye nidhamu zaidi katika Generation Z. Katika umri wako, tayari nilikuwa mtaani nikiwa na ndoa moja iliyofeli na uhusiano mmoja uliofeli, nikiwa na rundo la watoto mikononi mwangu, nikizunguka ulimwenguni kote na ufahamu mdogo wa jinsi itaisha. Lakini hapa uko, na kazi yako, biashara zako, nyumba yako nzuri ya joto, gari lako, na muhimu zaidi, wewe kama mtu. Nadhani wewe ndiye toleo la kile mama yangu alitaka, lakini hatima ilinichagua badala yake."

Mama huyo wa watoto watano aliendelea kueleza fahari yake kwa Vesha na kuzungumzia jinsi ambavyo amekuwa msukumo kwake.

Pia alieleza upendo wake mkubwa kwa msichana huyo mrembo na kumtia moyo kuendelea kusukuma.

"Unaposherehekea siku yako ya kuzaliwa leo, ujue unanitia moyo. Wewe ni mfano wangu. Mama, najua unapokea sehemu ya chuki kutoka kwa mashabiki wangu kwa kukanusha, na milango imepigwa usoni mwako kwa kuwa binti wa Akothee. Lakini jamani, mama, bado tunashinda kama familia. Jua tu kuwa ninakupenda sana na nitapanda milima kila wakati kwa ajili yako. Asante sana kwa kunikaribisha na kunipenda kwa kuwa mama yako,” aliandika.

Alimaliza barua yake kwa kumtakia tunda la kwanza la tumbo siku njema ya kuzaliwa.