Octoppizo amjibu vikali Khaligraph baada ya kumwita mwanamitindo na kudai kuwa hampendi

"Unachokitafuta utakipata haraka sana. Kunja kunja mdomo hio side ingine nani," Octo alimwambia Khaligraph.

Muhtasari

•Katika mahojiano, Khaligraph alidai kuwa msanii huyo mzaliwa wa Kibera hampendi licha ya kuwa hana tatizo naye.

•Octo alimuonya mpinzani kuwa chochote anachotafuta atakipata hivi karibuni na kumtaka azingatie mambo yake binafsi.

amemjibu Khaligraph baada ya kumtupia vijembe.
Octopizzo amemjibu Khaligraph baada ya kumtupia vijembe.
Image: INSTAGRAM//

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Henry Ohanga almaarufu Octoppizo hatimaye amevunja ukimya baada ya rapa mwenzake Khaligraph Jones kumtupia vijembe.

MAHOJIANO YA KHALIGRAPH

Katika mahojiano ya hivi majuzi na mtangazaji Oga Obinna, Khaligraph alidai kuwa msanii huyo mzaliwa wa Kibera hampendi licha ya kuwa hana tatizo naye.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Yes Bana’ alidai kuwa Octopizzo ameshikilia bifu yao inayodaiwa kuwa ya muda mrefu wakati yeye mwenyewe sasa akiwa amekomaa sana kuwa na uhasama dhidi yake.

“Huyo mvulana hajawahi kunipenda, unajua kuna tu mtu unahisi kama huwezi kumpenda na huwezi kumlaumu, damu tu zilikataa. Niliona kwa kusema kwamba hanipendi vile ninavaa. Mimi namuelewa kwa sababu mimi sihisi kama mimi nahisi hivyo kuhusu mtu mwingine yeyote, lakini namuelewa kwa sababu hata ningekuwa yeye singependa Khaligraph,” Khaligraph alisema.

Aliongeza, “Mimi sina uhasama na yeye, sina huo muda ukiona nimefikisha umri wa miaka 33, sasa vitu tulianza huko nyuma mpaka sasa hivi ni wapi na wapi, mimi nikikutana na Octo namsalimia 'niaje' akitaka aitike akitaka asiitike mimi nishamsalimia.”

Khaligraph aliendelea kudai kuwa rapa huyo mzaliwa wa Kibera ni mwanamitindo zaidi kuliko mwimbaji, kazi ambayo anamheshimia.

Rapa huyo mzaliwa wa Kayole hata hivyo alibainisha kuwa anaheshimu njia ya Octoppizo ya mafanikio, kutoka kwa kuzaliwa katika mtaa wa mabanda hadi kuwa rapa.

"Anafanya kazi nzuri, ana kurasa safi sana kwenye mitandao ya kijamii. Octo ni mwanamitindo mzuri sana, anapiga modeling fiti sana na namheshimu sana kwa kazi hiyo. Jamaa alikuja kutoka Kibera na namheshimu sana kwa sababu alikuja kutoka mazingira magumu sana lakini mambo ya nani anajua kurap kushinda mwingine huyo tuache,” Khaligraph alisema.

MAJIBU YA OCTOPIZO

Katika kile kilichoonekana kuwa jibu la moja kwa moja kwa Khaligraph, Octo kupitia akaunti yake ya Twitter alieleza kuwa kuna ‘baadhi ya watu’ ambao bado wanamzungumzia kwenye mahojiano.

Aliendelea kumuonya mpinzani wake huyo kuwa chochote anachotafuta atakipata hivi karibuni na kumtaka kuzingatia mambo yake binafsi.

“Naskia bado kuna fala flani aja acha kunitaja kwenye interview ma. Unachokitafuta utakipata haraka sana,” Octopizzo alisema.

Aliongeza, “Kunja kunja mdomo hio side ingine nani. Acha nimalizane na waterfalls kwanza.”

Mwimbaji huyo maarufu wa ‘Kamikaze, aliambatanisha ujumbe wake na video iliyomuonyesha akifurahia wakati kwenye maporomoko ya maji katika nchi ya kigeni.

Octoppizo na Khalighraph wanadaiwa kuwa na uhusiano mbaya na siku za nyuma walionesha uadui mkubwa kati yao hadharani.