"Pata nafasi moyoni unisamehe"Mchungaji Kiengei amuomba msamaha Pritty Vishy kwa matamshi ya chuki

Kiengei amekiri kwamba alitaja jina la Vishy kwa njia isiyo sahihi na kwamba alivuka mipaka kwa kauli mbaya alizotoa.

Muhtasari

•Kiengei amenyenyekea na kuomba msamaha kutoka kwa mtayarishaji maudhui Pritty Vishy kuhusu matamshi aliyotoa katika mahojiano.

•Mtumbuizaji huyo ambaye pia ni askofu aliahidi kutorudia kosa lilelile na akaendelea kumwalika Vishy kwenye kanisa lake.

Pritty Vishy na Bishop Kiengei
Image: HISANI

Mtumbuizaji maarufu wa Kikuyu na kiongozi wa kanisa Benson Gathungu almaarufu Kiengei amenyenyekea na kuomba msamaha kutoka kwa mtayarishaji maudhui Pritty Vishy kuhusu matamshi aliyotoa katika mahojiano ya hivi majuzi.

Jumanne asubuhi, mchekeshaji huyo alizamia kwenye mitandao yake ya kijamii na kuandika ombi la msamaha kwa mpenzi huyo wa zamani wa Stevo Simple Boy na kukiri kuwa alikosea kwa kauli alizotoa dhidi yake.

Kiengei alikiri kwamba alitaja jina la Pritty Vishy kwa njia isiyo sahihi na kwamba alivuka mipaka kwa kauli mbaya alizotoa.

“Prity Vishy, ​​samahani sana na nachukua muda huu kukuomba radhi sana kwa kutaja jina lako kwenye kipindi nilichopitia na kukutaja kimakosa, Pata nafasi moyoni mwako kunisamehe kwa kukuhutubia kwa njia isiyo sahihi, njia mbaya,” Kiengei alisema kupitia Facebook.

Mtumbuizaji huyo ambaye pia ni askofu katika kanisa moja maarufu jijini Nairobi aliahidi kutorudia kosa lilelile na akaendelea kumwalika Vishy kwenye kanisa lake.

"Hii haitatokea siku katika zijazo, naichukulia kama kosa langu, Pole dada yangu na karibu sana JCM CHURCH, KANISA LA WATU WOTE," alisema.

Haya yanajiri baada ya mtayarishaji maudhui huyo mwenye umri wa miaka 22 kuzamia kwenye mitandao ya kijamii kulalamikia kauli za Kiengei dhidi yake ambazo alizitaja kuwa za kudhalilisha mwili.

Huku akilalamika, Pritty Vishy alimkosoa askofu huyo na kutishia kwenda kanisani kwake siku ya Jumapili na kumkosoa mbele ya waumini wake.

Kwa nini ujifiche kanisani na kuchukua jina Askofu mkuu? unaonaje sasa umenitia aibu hadharani? unajua nina mama? unajua anajisikiaje kuhusu hili? wewe na wanafiki wengine wanaojificha makanisani ndio sababu tuliyoacha kukanyaga “nyumba ya bwana,” Pritty Vishy alilalamika.

Aliongeza, “Kwa kuwa ulifanya vizuri sana kunikumbusha kuwa mimi ni mbaya, sina mvuto na ni mnene, ambayo yote haya ni kweli🤷‍♀️ basi tukutane kanisani kwako, simama kwenye hiyo madhabahu, Mbele ya washiriki wa kanisa lako na wewe unapaswa kurudia maneno hayo yote….ili hata nijaribu sana jinsi gani, nitakumbuka mtu wa Mungu alisema kwamba mimi ni mbaya na sivutii…Ubarikiwe mtu wetu wa Mungu tuonane hivi karibuni katika nyumba ya Bwana.”

Watumiaji mtandao kadhaa, haswa wanawake, pia walikuwa wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumsapoti Pritty Vishy katika kulaani maneno mabaya dhidi yake.