Pritty Vishy afichua jinsi Stivo Simple Boy alivyokuwa anamcheza na wasichana wengine

Muhtasari

•Vishy alidai kuwa msanii huyo kutoka Kibra alikuwa na mazoea ya kutaniana na wasichana wengine kwenye simu.

•Vishy alisema kuchezwa na Stivo kulimuumiza sana kwa kuwa mahusiano yao haikuwa umefikia hatua ya uhusiano wa kimapenzi.

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy
Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy
Image: SAIDI ABDALLA

Pritty Vishy amemshtumu mpenzi wake wa zamani Stivo Simple Boy kwa kutokuwa mwaminifu wakati wa mahusiano yao.

Katika mahojiano na Obinna TV, Vishy alidai kuwa msanii huyo kutoka Kibra alikuwa na mazoea ya kutaniana na wasichana wengine kwenye simu.

Alidai kuwa tabia hiyo ya Stivo ilizua mzozo mkubwa kati yao na hatimaye akaamua kulipiza kisasi.

"Mimi nilijua tunachumbiana. Na yeye huko nje pia anachumbiana. Pia mimi niliona niende nichumbiane ndiyo tuwe 50/50," Vishy alisema.

Kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 alisema kuchezwa na Stivo kulimuumiza sana kwa kuwa mahusiano yao haikuwa umefikia hatua ya uhusiano wa kimapenzi.

Pia alimshtumu mwanamuziki huyo kwa kukosa kumwamini wakati wa mahusiano yao. Alisema Stivo alikuwa anamtilia shaka mwanaume yeyote ambaye angeonekana akitembea naye.

"Shida ya Stivo ata akiniona kwa barabara nikitembea na mjomba wangu jioni angekuja aniambie alisikia nilikuwa natembea na mwanaume. Nilishangaa kwani sifai kutembea na watu kwa sababu nachumbiana na yeye.Huyo ni mpenzi sumu," Vishy alisema.

Alikuwa anajibu madai ya Stivo kuwa aliwahi kutoka kimapenzi na wanaume wengi wakati wangali bado wanachumbiana.

Katika mahojiano ya hapo awali, Stivo alimshtumu mpenzi huyo wake wa zamani kwa kutoka kimapenzi na zaidi ya wanaume 50 wakati wa mahusiano yao. Alisema alijaribu kumuonya Vishy dhidi ya tabia hiyo ila akatia masikio yake pamba.

"Mimi nilinyamazia tu. Nilikuwa nikimwambia  kama ananipenda cha kweli awachane na hayo mambo yake. Nilimwambia akuwe na mtu mmoja ili tufunge ndoa. Lakini haeleweki jameni," Alisema.

Stivo aliweka wazi kuwa hana mpango wowote wa kuwahi kurudiana na Vishy huku akidai kuwa alitenda makosa mengi kiasi cha kutostahili msamaha.

Vishy kwa upande wake ameweka wazi kuwa kutengana kwao kulikuwa kwa pande zote. Alisema kuwa bado anatafuta mtu mwingine wa kuchumbiana naye.