Pritty Vishy ahuzunika baada ya kukejeliwa kwa kudhulumiwa kimapenzi na babake akiwa mdogo

Pritty Vishy alisema hawezi kujigamba kuhusu kunajisiwa na akabainisha kuwa hakufurahia kamwe kupitia hali hiyo.

Muhtasari

•Jamaa alimshutumu Vishy kwa kuwa na kiburi huku akiwakumbusha watu kuwa hapo awali aliwahi kukiri kudhulumiwa kimapenzi na babake.

•Pritty Vishy aliwahi kufunguka kuhusu jinsi babake mnyanyasaji alivyojaribu kumnajisi mara kadhaa alipokuwa katika shule ya msingi.

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy
Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy
Image: SAIDI ABDALLA

Mtayarishaji maudhui mashuhuri wa Kenya Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy alijawa na hisia baada ya mtumiaji wa mtandao wa Instagram kufanya mzaha kuhusu kukiri ushuhuda wake wa hapo awali ambapo alifichua kuwa babake wa kambo alijaribu kumnajisi.

Katika sehemu ya maoni ya moja ya posti zake ya Instagram, jamaa alimshutumu mpenzi huyo wa zamani wa Stivo Simple Boy kwa kuwa na kiburi huku akiwakumbusha watu kuwa hapo awali aliwahi kukiri kudhulumiwa kimapenzi na babake.

“Huyu si ni yule dame alisema alikuwa akid*nyw* na baba yake akiwa class 3.. saa hii ni kiburi tu,” baringo_west_niccur aliandika chini ya chapisho la Prittty Vishy.

Huku akijibu maoni ya mtumiaji wa Instagram, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alisema kwamba alipoteza maneno kabisa baada ya kuyasoma.

Pritty Vishy alishangaa kwa nini mtu angefikiri alikuwa akijiganba kuhusu kunajisiwa na akabainisha  kwamba hakuwa na furaha kamwe kupitia yale aliyopitia utotoni.

“Wow! Wow tu. Hii ilinipata na sina la kusema kusema ukweli. Kwa hiyo baadhi ya watu wanadhani kuwa kunajisiwa ni jambo la kujivunia? Au unadhani nimefurahi kwa sababu nilikuwa kwenye kiatu hicho? Ni chungu kuandika vile naapa lakini hata hivyo..” aliandika.

Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Katika mahojiano na Mpasho mwaka jana, Pritty Vishy alifunguka kuhusu jinsi babake mnyanyasaji alivyojaribu kumnajisi mara kadhaa alipokuwa katika shule ya msingi.

“Baba yangu wa kambo alijaribu kuninajisi nikiwa darasa la tatu, lakini ujasiri ulinisaidia. Kila usiku nilikuwa nikikimbia na kwenda kulala kwa bibi yangu,. Hata iweje, ni heri niende tu, nilikuwa najifanya naenda kukojoa na hivyo ndo mimi napotea,” Pritty Vishy alisimulia.

Aliongeza, “Mama yangu akajua mpango wangu ni kujifanya naenda kukojoa, akanishika. Nikaanza kujifanya wakati amelala hivi, na mimi nafunga mlango natoka naenda. Mama alijua hatimaye na alinichapa, alinipasua kwenye paji la uso juu alikuwa ananipiga na mbao. Aliponipasua ndio nilimwambia. Aliposikia alitupa mbao chini akaanza kulia. Alifaa kwenda kibarua akaanza kulia. Hiyo ndio ilikuwa wakati mbaya zaidi.

Baada ya hapo, mama akajaribu kumuuliza baba hadi akaita familia. Familia ya baba wa kambo ikasema mimi najaribu kuvunja ndoa ya mamangu kwa hivyo hawakufanya chochote. Juu mama yangu amezaa watoto wawili na huyo mwanaume, dada yangu mlemavu na kaka yangu, hakuenda. Ilibidi akae angalau aone kama anaweza kubadilika. Nikiwa katika darasa la tano akarudia kitendo hicho hicho kwa hivyo nikiwa class seven ikabidi nimepelekwa Children’s home kwa sababu ilikuwa imezidi sana. Nikiwa darasa la nane tena tukapigana akanipiga ngumi ya matiti hadi nikaenda nikafanyiwa scanning. Mama yangu akaona huyu ataniulia mtoto ikabidi sasa tumehama.”

Pritty Vishy alifichua kwamba baba huyo wa kambo alikamatwa mara moja kutokana na suala hilo lakini aliachiliwa baada ya wiki moja baada ya kudai kuwa alikuwa amebadilika ilhali hakuwa amebadilika.