Rais Samia amtafuta Diamond kwenye hafla ya Harmonize, atoa hotuba nzito ya kusisimua

Rais Samia alipata kutangamana na mamake Harmonize na kumpongeza kwa kazi kubwa ya kumlea.

Muhtasari

•Idadi kubwa ya wageni waalikwa walipamba hafla hiyo ya kupendeza ambayo ilihudhuriwa hata na rais Samia Suluhu Hassan.

•Rais aliwapongeza wasanii wengine wa taifa hilo kwa mchango wao mkubwa na athari wanazoleta akibainisha kuwa nao wanazidi kukua.

akimsalimia Rais Samia Hassan
Harmonize akimsalimia Rais Samia Hassan
Image: INSTAGRAM/// KONDEGANG

Siku ya Jumamosi, staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize aliandaa hafla kubwa ya kuzindua albamu yake ya tano kwenye ukumbi wa Milimani City jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Idadi kubwa ya wageni waalikwa wakiwemo wasanii tajika walipamba hafla hiyo ya kupendeza ambayo ilihudhuriwa hata na rais Samia Suluhu Hassan.

Wakati akiwahutubia wageni katika hafla hiyo, Rais Samia ambaye alikuwa mgeni mkuu aliipongeza albamu ya mwimbaji huyo na ukuaji wake.

“Nilikuwa namuangalia Harmonize. Nikamvuta Harmonize wa miaka, sita, minane nyuma, na alivyo leo. Amenifurahisha sana, sana. Unamuona Harmonize aliyekua,” Rais Samia Hassan alisema.

Kiongozi huyo wa Tanzania pia aliwapongeza wasanii wengine wa taifa hilo kwa mchango wao mkubwa na athari wanazoleta akibainisha kuwa nao wanazidi kukua.

Rais alitaja kuwa kuna changamoto nyingi ambazo wasanii wamepambana nazo kabla ya kufanikiwa lakini akawahimiza kutokata tamaa.

“Vijana wangu wengi wanapita hapo, kina Rayvanny.. Rayvanny yupo? Ommy yupo, Dimpoz? Naseeb yupo? Hayupo.. lakini wengi wanapita kwenye mapito hayo. Kwa hiyo na wametulia,” alisema.

Rais Samia alipata kutangamana na mama wa bosi huyo wa Konde Music Worldwide na kumpongeza kwa kazi kubwa ya kumlea, jambo ambalo Harmonize alijivunia.

Wakati akieleza hisia zake kuhusiana na tukio la mama yake kukutana na rais, Harmonize alishindwa kuficah furaha yake na kutaja kipindi hicho kuwa ni ndoto.

“Usiniamshe, ndoto tamu zaidi kuwahi kutokea 005,” aliandika Harmonize kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha maelezo yake na picha ya mama yake akimsalimia raisi Samia.

Konde Boy alikuwa amewaalika Watanzania wengi mashuhuri, wakiwemo waimbaji bora nchini humo kwa hafla yake ya Jumamosi.

Alikuwa amemualika hata bosi wake wa zamani Diamond Platnumz, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisemekana kuwa na beef  naye. Diamond na hasidi wake mkuu Alikiba hata hivyo hawakuonekana kwenye tukio hilo.

Mwenzake wa zamani katika WCB, Rayvanny hata hivyo alihudhuria hafla hiyo ya kupendeza.