Rayvanny adokeza majuto kufuatia kuachana na Paula Kajala

Staa huyo alichapisha picha ya kumbukumbu ya siku zake na Paula.

Muhtasari

•Staa huyo wa Bongo alichapisha picha ya kumbukumbu ya siku zake na Paula kwenye ukurasa wake wa Facebook.

•Emoji hiyo pengine ilikusudiwa kufupisha hisia zake za jumla kuhusu uhusiano wao uliovunjika.

katika picha ya kumbukumbu.
Rayvanny na Paula Kajala katika picha ya kumbukumbu.
Image: FACEBOOK// RAYVANNY

Kuna uwezekano mkubwa kuwa staa wa Bongo, Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny bado anakumbuka mahusiano yake na Paula Kajala.

Siku ya Jumatano jioni, bosi huyo wa Next Level Music alichapisha picha ya kumbukumbu ya siku zake na Paula kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Rayvanny aliambatanisha picha hiyo yake na binti huyo wa muigizaji mkongwe Kajala Masanja wakiwa wameketi kwenye kiti na emoji ya uso uliofunikwa kwa kiganja cha mkono ambayo mara nyingi huashiria  kufadhaika au aibu.

Ingawa hakushiriki maelezo zaidi, emoji hiyo pengine ilikusudiwa kufupisha hisia zake za jumla kuhusu uhusiano wao uliovunjika.

Mwaka jana wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania, Rayvanny alidokeza kusambaratika kwa mahusiano yake ya muda mrefu na mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20.

Alidokeza hayo wakati akitumbuiza wimbo wake 'Naogopa' ambapo aliongeza mistari kadhaa iliyosikika kama ujumbe wa kukiri.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Baadaye, msanii huyo wa zamani wa WCB alidaiwa kuzozana na Paula, madai ambayo alipuuzilia mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Staa huyo aliweka wazi kuwa amejikita tu kwenye muziki na hakuwa na ubishi na mwanamke yeyote yule kote duniani.

Aikuwa akijibu tuhuma za kumshambulia binti huyo wa muigizaji Fridah Kajala Masanja katika wimbo wake mpya wa 'Tusipanganie'.

"Mbona Paula hana habari nawe, wewe kutwa vijembe, vijembe.. fanya muziki," shabiki mmoja alimwambia Rayvanny chini ya video moja ambayo alichapisha kwa ajili ya kutangaza wimbo huo ambao aliomshirikisha Gnako.

Katika wimbo huo, msanii huyo wa zamani wa WCB alisikika kutuma ujumbe kwa mwanamke asiyetaja jina ambaye tayari ameshaachana naye, sababu tosha ya baadhi ya mashabiki kuamini kwamba alimzungumzia Paula.

Rayvanny hata hivyo katika jibu lake aliweka wazi kuwa maneno ya wimbo huo hayakumhusu yeyote bali alikuwa akifanya muziki tu.

"Nyamaza! Ninafanya muziki wangu kwa ajili ya watu wangu, ninatengeneza vibao kwa ajili ya mashabiki wangu na sina vita na mwanamke yeyote duniani. #tusipangiane," alijibu kwa hasira.