Rayvanny amfichulia Paula kwa nini alimtema huku wakitupiana matusi mazito hadharani

Rayvanny alisisitiza alimtafuta mwanamitindo huyo kwa ajili ya mapenzi na kumpongeza kwa mahusiano yake ya sasa.

Muhtasari

•Wasanii hao wawili wa bongo walinyoosheana vidole kuhusu mahusiano yao yaliyovunjika mwaka jana.

•Paula alidai kuwa Rayvanny hakuwa mwaminifu kwani angem'cheat na mzazi mwenzake, Fahyma mara kwa mara.

Rayvanny ajuta kumpenda Paula
Rayvanny ajuta kumpenda Paula
Image: MAKTABA

Jumatatu, waliokuwa wapenzi, Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny na Paula Kajala walishiriki vita mtandaoni huku wakirushiana matusi mazito.

Wakati wa mzozo wao kwenye Instagram, wasanii hao wawili wa bongo walinyoosheana vidole kuhusu mahusiano yao yaliyovunjika mwaka jana.

Rayvanny ambaye hivi majuzi alirudiana na mzazi mwenzake, Fahyma alidai kwamba binti huyo wa muigizaji Kajala Masanja alimsaliti kimapenzi na nduguye.

"Nilijua unalala na kakangu niliyemheshimu sana kwenye mziki wangu na unajua tunaheshimiana sana, hapo ndipo nilibadilisha mawazo," Rayvanny alisema.

Paula hata hivyo alibainisha kwamba hakuwahi kumsaliti bosi huyo wa Next Level Music wakati wa mahusiano yao ya mwaka mmoja.

Aidha, alidai kuwa mwenzake Rayvanny hata hivyo hakuwa mwaminifu kwani angem'cheat na mzazi mwenzake, Fahyma.

"Nilikaa na wewe mwaka mzima kila mtu anajua tumeachana wakati ulikuwa na mimi na mwanamke wako. Ulitaka niendelee kukaa na wewe wakati unanificha  ficha ukienda kwa mwanamke wako unasema nakusumbua, ukija kwangu unasema mwanamke wako anakusumbua," Paula alijibu.

Mwanamitindo huyo wa miaka 20 alimbainishia Rayvanny kuwa alifahamu matendo yake na ndiposa akachukua hatua ya kumuacha.

"Acha kufanya watu waonekane mbaya. Unajua nilijitolea vingapi kwaajili ya haya mahusiano?? Mbona husemi marafiki zangu ulivyolala nao kwenye gari lako," Paula alimuuliza mpenzi huyo wake wa zamani.

Paula alimtaka mwanamuziki huyo kukoma kumchafulia jina kwa madai mazito dhidi yake na kumwagiza atoe ushahidi wowote kuthibitisha kwamba alimsaliti kimapenzi na ndugu huyo wake asiyefichuliwa. Alidai kwamba Rayvanny aliwahi kumsaliti na baadhi ya marafiki zake pamoja na wapenzi wa marafiki wake.

Rayvanny kwa upande wake alisisitiza alimtafuta binti huyo wa Kajala kwa ajili ya mapenzi na kumpongeza kwa mahusiano yake ya sasa.

Wiki chache zilizopita, mamake Paula, Kajala Masanja aliweka wazi kwamba hakufurahi wakati alipogundua kwamba binti yake yupo kwenye mahusiano na Rayvanny takriban miaka miwili iliyopita.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha humu nchini, Kajala alisema pia yeye alikuja kufahamu kuhusu mahusiano hayo kupitia mitandao ya kijamii kama wanamitandao wengine wote.

"Paula hata hakuwa na nguvu za kuniambia. Ilitokea tukaona huko mitandaoni. Alikuwa 18. Kwa mawazo yangu nilijua Paula hana mpenzi," alisema.

Kajala alikiri kwamba alijaribu sana kumshauri mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 dhidi ya mahusiano na bosi huyo wa Next Level Music lakini juhudi zake  ziliangukia patupu kwani Paula hakusikia.

"Nilijaribu sana kumweleza kwamba hii sio sahihi lakini mtu anaenda anafanya kinyume, inabidi umeacha tu. Ukimwambia asiende na huyo mtu anasema sawa lakini bado anaendelea. Nilijaribu kumzuia sana," alisema.

Aidha, alisema baada ya kushindwa kumshauri Paula dhidi ya uhusiano huo, alimshauri jinsi ya kujiendeleza katika mahusiano.

"Nilimwambia kwa sababu yeye bado ni mdogo atulie bado ana maisha mbele. Asifanye vitu kwa hasira," alisema.

Kajala alisema alifurahi wakati mahusiano ya bintiye na Rayvanny yaligonga mwamba kwa sababu hakuona ndoa pale.