Ringtone Apoko amshtumu King Kaka kwa kusaini wasanii mashoga

Amemtaka King Kaka kukatiza uhusiano na na wasanii hao ambao amedai ni mashoga.

Muhtasari

•Ringtone alidai kwamba kumekuwa na tetesi kuwa wasanii wake wa kike waliosainiwa na rapa huyo wanavutiwa na wanawake wenzakeo kimapenzi.

•Haya yanajiri huku kukiwa na mjadala mkubwa unaoendelea humu nchini kuhusu suala tata la wapenzi wa jinsia moja.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA, RINGTONE

Mwenyekiti wa muungano wa wasanii wa injili nchini Kenya wa kujitangaza, Alex ‘Ringtone’ Apoko amemshutumu mwanamuziki mwenzake Kennedy Ombima almaarufu King Kaka kwa kusajili wasanii mashoga.

Akizungumza kwenye video fupi aliyochapisha kwenye Instagram, Ringtone alidai kwamba kumekuwa na tetesi kuwa wasanii wake wa kike waliosainiwa na rapa huyo wanavutiwa na wanawake wenzakeo kimapenzi.

Mwimbaji huyo wa injili sasa anamtaka King Kaka kujibu madai hayo na kueleza msimamo wake kuhusu mapenzi ya jinsia moja.

"King Kaka kwa sababu tunakujua kama mtu wa familia, mtu mzuri mwenye roho safi, tunataka uweke wazi kwamba husapoti ushoga,"  Ringtone alimwambia rapa huyo katika video ambayo alipakia siku ya Alhamisi.

Mwimbaji huyo wa injili aliyezingirwa na utata mwingi pia alimtaka King Kaka kukatiza uhusiano na na wasanii hao ambao alidai ni mashoga. 

Haya yanajiri huku kukiwa na mjadala mkubwa unaoendelea humu nchini kuhusu suala tata la wapenzi wa jinsia moja. Wakenya wengi wakiwemo wanasiasa wakuu na wasanii wameendelea kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.

Siku ya Jumatano, mjasiriamali wa vipodozi, Michelle Ntalami alilazimika kufafanua kuhusu uhusiano wake na msanii wa Kaka Empire yake King Kaka, Fena Gitu, kufuatia picha zao za pamoja zilizosambaa wiki jana.

Wengi ambao walichanganua picha hizo walihisi kuwa huenda wawili hao ni wapenzi wasagaji kwa jinsi walivyokuwa lakini Ntalami alikanusha madai hayo vikali huku akisema kwamba Gitu kwa muda mrefu amekuwa rafiki wa karibu ambaye wameshirikiana naye katika kufanikisha mambo tumbi nzima.

“Chenye naweza sema ni kwamba Fena ni rafiki mmoja mzuri sana kwangu na hakuna kinachoendelea kimapenzi baina yetu. Kwa wale ambao wanatujua au pengine tumewahi kutana nao mnaweza gundua kuwa urafiki wangu na Fena ulianza kutoka Instagram, tumefanya miradi mingi pamoja. Tumefanya video za muziki naye, amekuwa balozi wa mauzo kwa bidhaa zangu kwa muda mrefu tu,” Ntalami alisema katika mahojiano na kituo kimoja cha redio humu nchini.