"Saa hii hakuna pesa!" Eric Omondi akubali kazi ya kijakazi aliyopewa na Ringtone, atoa masharti

Mchekeshaji huyo aliweka wazi kuwa yupo tayari kuchukua ofa hiyo na kuanza kazi mara moja.

Muhtasari

•Ijumaa wakati akiwa kwenye mahojiano na NTV, Ringtone alisema amejitolea kumuajiri Eric Omondi nyumbani kwake Runda, Nairobi.

•Eric alisema ingawa amekubali kazi hiyo, ni sharti mwimbaji huyo ampeleke katika makazi yake ya  Runda anayodai kumiliki.

Ringtone Apoko na Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Eric Omondi ameeleza kuvutiwa kwake na kazi ya mtunza bustani aliyopewa na msanii wa nyimbo za injili Ringtone Apoko.

Ijumaa wakati akiwa kwenye mahojiano na NTV, Ringtone alisema amejitolea kumuajiri Eric Omondi nyumbani kwake Runda, Nairobi.

Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wasanii wa Injili wa kujibandika alidokeza kuwa Bw Omondi amelemewa kabisa  na usanii.

"Siku ingine nilimwambia akuje kwangu Runda nimuajiri kazi akakataa. Naweza kumwandika awe msimamizi wa kiwanja, hakuna kitu ingine. Eric Omondi hata talanta, labda naweza kumwandika kama kijakazi," alisema.

Katika mahojiano na Vincent Mboya, Eric aliweka wazi kuwa yupo tayari kuchukua ofa hiyo na  kuanza kazi mara moja.

"Nimekubali ofa hiyo. Naweza kuanza kazi siku ya Jumatatu, anipatie 50, 000 mimi nitaenda Runda," alisema.

Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na utata alibainisha kwamba Ringtoneamezoea utani na uwongo kwa miaka mingi.

Alisema ingawa amekubali kazi hiyo, ni sharti mwimbaji huyo ampeleke katika makazi yake ya  Runda anayodai kumiliki.

"Nimekubali hiyo kazi kwa sababu hakuna Runda, jamaa anaishi South C. Ni lazima kazi ikuwe Runda sio South C. Lazima iwe mahali kuna bustani, nataka penye kuna nyasi, asinipeleke kwa 2 bedroom yake," alisema.

Wakati akitoa ofa ya kazi kwa Bw Omondi, Ringtone alibainisha kuwa mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 40 hawezi  kumudu kuishi katika mtaa wa kifahari wa Runda kama vile yeye. Alisema iwapo Omondi atakubali ofa yake ya kazi  basi yupo tayari kumpatia mshahara wa Ksh 50,000 kila mwezi.

"Anatamani maisha mazuri.Akuje nimpatie kazi ya mjakazi. Bila hivyo hawezi kuishi Runda. Naweza kumlipa 50,000. Hiyo ni pesa kidogo sana," alisema kabla ya kuonyesha noti za elfu moja alizokuwa nazo mfukoni.

Mwimbaji huyo alidai kuwa jumla ya pesa ambazo alikuwa amebeba katika studio za NTV ni shilingi laki moja.

Omondi hata hivyo alidai kuwa mwenyekiti huyo wa muungano wa wasanii wa injili wa kujibandika amekuwa akibeba pesa zila kwa kwa miaka kadhaa. Alisema  ni za maonyesho tu na hata sio zake.

"Amekuwa nayo tangu 2017, huwa anatembea nayo kwa mfuko. Ni ya Jaguar. Ni halisi lakini sio zake. Ni za Jaguar, huwa anatembea nazo alafu baada ya kuonyesha anazirudisha," alisema mchekeshaji huyo.

Mchekeshaji huyo alisema yupo tayari kuanza kazi bila kupokea pesa zozote na kusubiri malipo baada ya mwezi.