Samidoh ajibu kwa kejeli kuhusu kumpenda Karen Nyamu kwa sababu ya utajiri wake, kupewa pesa naye

Mwanamuziki huyo alishtumiwa kwa kupewa pesa na seneta Nyamu ambaye ni mama ya watoto wake wawili.

Muhtasari

•Mwanamitandao alidai kuwa hata baadhi ya wanaume huchumbiana na wanawake kwa sababu ya pesa zao na akadai kuwa mwimbaji huyo wa Mugithi ni miongoni mwao.

•Katika majibu yake, mwimbaji huyo alimtaka mwanamitandao huyo pia kutafuta pesa nyingi za kugawana na mumewe mara kwa mara.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Mwimbaji maarufu wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alijibu kwa utani baada ya kushtumiwa kwa kuchumbiana na Seneta Karen Nyamu kwa sababu ya pesa zake.

Baba huyo wa watoto watano alikuwa ameweka chapisho kuhusu jinsi wanaume wasio na pesa wanavyohukumiwa tofauti na wanawake walio katik hali kama hiyo katika jamii wakati shutuma hizo zilipoibuka.

Katika chapisho lake, mwanamuziki huyo wa nyimbo za Kikuyu alikuwa amebainisha kwamba wanaume wanaishi kujitegemea wao wenyewe ilhali mwanamke anaweza kufaidika kifedha kwa kuwa tu na mwanamume.

"Mwanamke maskini bado ni mwanamke. Mwanamke mwenye elimu bado ni mwanamke. Mwanamke ambaye hawezi kukidhi mahitaji bado ni mwanamke. Na anapata heshima yote anayostahili. Lakini mwanamume asiye na vitu hivi ni mzigo hata kwa familia yake,” Samidoh aliandika kwenye Facebook.

Aliongeza, "Maisha ya wanaume yanategemea wao tu. Ikiwa huna kazi, unalala njaa, hakuna bahati, hakuna wa kukuhurumia, ni kazi ngumu tu. Mwanamke anaweza kupata njia yake ya kutoka lakini mwanamume lazima afanye kazi kwa bidii. Mungu awe anawabariki mkienda kutafuta.”

Baadhi ya wanamitandao hasa wanaume walikubaliana na hisia zake huku wengine wakitofautiana naye na hata kufanya zaidi kumkosoa.

Kwenye sehemu ya maoni, mtumiaji mmoja wa Facebook alidai kuwa hata baadhi ya wanaume huchumbiana na wanawake fulani kwa sababu ya pesa zao na hata akadai kuwa mwimbaji huyo wa Mugithi ni miongoni mwao huku akidai kuwa huwa anapewa pesa na mpenzi wake Karen Nyamu.

"Pia wanaume wanaweza kufaidika unamaanisha, pia wewe si ulipenda Karen juu ya pesa. Na usitudanganye Karen hakupeangi doo," Mama Natashia alimjibu.

Katika majibu yake, mwimbaji huyo alimtaka mwanamitandao huyo pia kutafuta pesa nyingi za kugawana na mumewe mara kwa mara.

"Hehe, pia wewe tafuta pesa kwa bidii ili uwe unapatia mume wako. Usiwe kilema mwili na pia akilini wamaitu😂," alijibu Samidoh.

Msanii huyo amekuwa kwenye mahusiano na seneta Karen Nyamu kwa miaka kadhaa sasa na wawili hao tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja. Mapenzi yao yameonekana kunoga zaidi katika miezi ya hivi majuzi hasa baada ya mke wa kwanza wa Samidoh, Edday Nderitu kuhamia Marekani mapema mwaka huu.