Seneta Karen Nyamu akiri kutatizika kufanya kazi kwenye baridi akikumbuka alimuacha Samidoh kitandani

Nyamu alikiri kuwa haikuwa rahisi kwake kumakinika na kazi akikumbuka alimuacha mpenzi wake kitandani.

Muhtasari

•Seneta Karen Nyamu ameshiriki ungamo la kusisimua kuhusu jinsi ilivyokuwa ngumu kwake kuzingatia kazi katika hali ya baridi.

•Ni dhahiri kwamba mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata alikuwa akimzungumzia mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Siku ya Jumatano, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alishiriki ungamo la kusisimua kuhusu jinsi ilivyokuwa ngumu kwake kumakinika kazini katika hali ya baridi.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Facebook, Nyamu alishiriki picha zake kadhaa akiwa kazini na baadhi ya wenzake ambapo alionekana akipitia nyaraka.

Katika sehemu ya maelezo, mama huyo wa watoto watatu alikiri kuwa haikuwa rahisi kwake kumakinika na kazi akikumbuka alimuacha mpenzi wake kitandani.

"Mimi nikijaribu kumakinika kazini na hii baridi nikikumbuka tu niliwacha mlook-alike, mscorpio wangu kwa kitanda, haha," seneta Nyamu alisema kwenye picha alizochapisha.

Ingawa hakutaja majina, ni dhahiri kwamba mwanasiasa huyo mtata alikuwa akimzungumzia mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Siku chache zilizopita, mwimbaji huyo wa Mugithi alimuita Karen Nyamu majina yale yale seneta huyo aliyotumia katika posti yake wakati akimtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Mapema mwezi huu, Samidoh aliimposti mpenzi wake Karen Nyamu na kumsherehekea vizuri kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwimbaji huyo ambaye kwa muda mrefu amejaribu kuficha mahusiano yao kutoka kwa umma aliamua kumsherehekea hadharani mama huyo wa watoto wake wawili mnamo siku yake maalum ambapo alikuwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake kwa mpenziwe, Samidoh alimtambulisha kama ‘pacha’ wake na kukiri kwamba seneta huyo ndiye ‘scorpio’ anayempenda zaidi (mtu aliyezaliwa kati ya Oktoba na Novemba).

"Mtu tunayefanana, scorpio kipenzi," Samidoh aliandika kwenye picha yake na seneta Nyamu.

Mwimbaji huyo aliendelea kuweka wazi kwamba alikuwa tayari kutoficha uhusiano wao tena.

"Sitacheza salama. Heri ya kuzaliwa @senatorKarenNyamu,” aliandika.

Mwanamuziki huyo pia alitumia moja ya nyimbo zake za mapenzi kutuma ujumbe maalum kwa mama huyo wa watoto wake wawili.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, seneta Nyamu aliifunguka kuhusu jinsi mpenzi wake Samidoh anavyomuonyesha mahaba tele ikiwa ni pamoja na kumnunulia maua na kwenda naye katika maeneo ya burudani.

"Huwa ananunua maua, ananiambia anakuja kunichukua, tunaenda mahali kuna muziki tunakula, tunakunywa cocktails, tunacheka, sisi wawili tu alafu tunaenda nyumbani," Karen Nyamu alifichua.

Huku akizungumzia sifa anazopenda kwa mpenzi huyo wake, Nyamu alimsifu na kufichua kuwa ana vibe ya kuvutia sana ambayo anaipenda.

“Yupo poa, ana roho poa, anachekesha sana, ni muwazi, hajidai, roho iko uchi unaona. Ana vibe ambayo sijawahi kuona maishani mwangu. Anavutia sana. Kwa kawaida huwa anasema baadhi ya mambo na najua maishani mwangu sitawahi kusikia mtu mwingine akiyasema. Kwa kawaida mimi humwambia hivyo," Nyamu alisema.