Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amesisitiza kuwa madai ya hivi majuzi ya kuwa na michubuko jichoni baada ya kupigwa na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidah ni ya uwongo.
Katika mahojiano na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kuwa hakuhusika katika vita na baba huyo wa watoto wake wawili wadogo.
Nyamu alidokeza kuwa mwimbaji huyo wa Mugithi hajawahi kumshambulia tena tangu ilipodaiwa kutokea kwa mara ya kwanza mwaka wa 2021.
"Sijui watu walijifanya au walijua, walisisitiza kuwa nimepigwa na tumepigana. Hapana, hatukuwa tumepigana. Tangu jambo hilo litokee kwa mara ya kwanza, halijatokea tena,” Karen Nyamu alisema.
Wakili huyo alibainisha kuwa mpenzi wake alijifunza kutokana na tukio la kumpiga lililodaiwa kutokea takriban miaka miwili iliyopita na amekuwa mpole tangu wakati huo.
“Sam ni mtu anayejifunza haraka na kujuta. Alijifunza na hutawahi kuona kitu kama hicho tena. Kwa mfano, zamani tulikuwa tunapigania watoto lakini utamwona amejifunza na kufanya vizuri. Kuna mambo ambayo hajui, lakini baada ya kujua, yeye ni mwanafunzi wa haraka. Hatukuwahi kupigana,” alisema.
Nyamu pia alipuuzilia mbali maoni ya mzazi mwenza mwingine wa mwimbaji huyo wa Mugithi, Edday Nderitu kuhusu kisa cha madai ya kushambuliwa mwezi uliopita na akabainisha kuwa pia yeye anafahamu kuwa baba huyo wa watoto wao hajakuwa mwenye vurugu tangu 2021.
Mwishoni mwa mwezi Juni, picha ya seneta huyo wa UDA akionekana kuwa na jicho lenye mchubuko ilivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuibua madai kuwa alipigana na mzazi mwenzake Samidoh.
Picha hiyo ilipigwa alipokuwa ameungana na spika wa seneti Amason Kingi na viongozi wengine kwa hafla ya skauti katika kaunti ya Nyeri.
“Ukiangalia picha zingine za siku hiyo, sikuwa na jeraha la jicho,” Karen alisisitiza.
Mwezi Agosti 2021, Nyamu alimshutumu Samidoh kwa kumpiga na kuvunja simu yake.
Alidai kuwa alishambuliwa wakati akiwa na ujauzito wa miezi mitatu wa mtoto wao wa pili.