"Shida yake ni kunywa uji sana" Nameless alalamika kuhusu Wahu, aeleza kwa nini anaonekana mjamzito

Alisema tayari wamefunga mlango wa kuzaa na kuweka wazi kuwa hawana mpango wa kuongeza mtoto mwingine.

Muhtasari

• Nameless aliweka wazi kuwa mwili wa mkewe unaoonekana kuwa mkubwa kupita kawaida kutokana na kula vizuri na kuwa na amani.

“Hamna bao hapo. Hiyo tumefunga sasa. Unataka niwe baba Abraham. Hiyo Imeisha?” alisema.

katika hafla ya King Kaka.
Wahu na Nameless katika hafla ya King Kaka.
Image: INSTAGRAM//

Mwimbaji mkongwe wa Kenya David Mathenge almaarufu Nameless amesisitiza kuwa mkewe, Wahu Kagwi hana ujauzito, kinyume na madai ambayo yamekuwepo.

Siku ya Jumatatu, rapa King Kaka alichapisha picha ya Nameless na Wahu ambayo ilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kwani tumbo la mama huyo wa watoto watatu likionekana kuchomoza kupita kawaida.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Nameless hata hivyo aliweka wazi kuwa mwili wa mkewe unaoonekana kuwa mkubwa kupita kawaida kutokana na kula vizuri na kuwa na amani.

“Nikula tu vizuri tu, na kutulia. Hiyo imeisha! Hakuna kitu, ni chakula tu amekula vizuri na kutulia,” Nameless alisema.

Baba huyo wa mabinti watatu aliendelea kufichua kuwa mkewe amekuwa akinywa uji mwingi kutokana na kumnyonyesha mtoto wao mdogo, hivyo kuchangia kuongezeka kwa uzito wake.

Hata hivyo, alitangaza kuwa hivi karibuni Wahu ataanza kufanya mazoezi ya viungo kwenye chumba cha mazoezi katika juhudi za kupunguza uzani wake.

“Hamna mimba, hamna ni chakula tu.. anarudi gym. Anakunywa tu uji nyingi, shida yake ni kukunywa uji sana. Anakunywa uji nyingi kwa sababu ya Shiro,” alisema.

Mwanamuziki huyo mkongwe alibainisha kuwa tayari wamefunga mlango wa kuzaa na kuweka wazi kuwa hawana mpango wa kuongeza mtoto mwingine.

“Hamna bao hapo. Hiyo tumefunga sasa. Unataka niwe baba Abraham. Hiyo Imeisha?” alisema.

Takriban miezi miwili iliyopita, Wahu alifunguka kuhusu changamoto ya kuongezeka kwa uzani wa mwili wake tangu alipozaa mtoto wake wa tatu mwaka jana.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Sweet Love' katika mahojiano na Eve Mungai alisema kuwa wakati huo mwili wake ulikuwa umeongeza uzani kwa kasi ya ajabu na alikaribia kufikisha kilo 90.

Wahu alisema kuwa mwanzoni alikuwa mdogo lakini miezi michache baada ya kujifungua, alijipata akiongeza uzani wa takribani kilo 30.

“Kitu cha muhimu ni kujipenda jinsi ulivyo. Mimi nimeongeza uzani mwingi, si kidogo. Rafiki yangu niko karibia kilo 90, nyuma nilikuwa kadogo lakini sasa nimeongeza takribani kilo 30 sasa hivi na niko sawa binafsi kwa sababu najua sababu, ni mwili wangu na muda wa kupunguza uzani utafika tu, itu muhimu ni kujipenda jinsi ulivyo na kuikumbatia hali yako,” Wahu alisema.

Aidha, alisema kuwa amepunguza kasi ya kufanya miradi ya muziki kwa sasa katika kile alisema kuwa ni kujitolea kuwa mama bora kwa mwanawe Shiru hadi pale atakapomaliza kunyonya na mambo mengine yatatokea tu.