"Siko tayari kwa thieta!" Diana Marua aeleza wasiwasi huku akidokeza kujifungua hivi karibuni

Mke huyo wa Bahati alifichua kuwa anakaribia kwenda hospitali kupokea zawadi ya mtoto wake wa tatu.

Muhtasari

•Mke huyo wa Bahati alifichua kuwa  anakaribia kwenda hospitali kupokea zawadi ya mtoto wake wa tatu.

•Diana alieleza hamu yake kubwa ya kukutana na mtoto wake wa tatu.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Muunda maudhui mashuhuri Diana Marua amedokeza kuwa tarehe ya kujifungua mtoto anayebeba tumboni kwa sasa iko karibu.

Katika chapisho lake la hivi punde kwenye Instagram, mke huyo wa msanii Kelvin Kioko almaarufu Bahati alifichua kuwa  anakaribia kwenda hospitali kupokea zawadi ya mtoto wake wa tatu.

"Huu umekuwa ujauzito wangu mfupi zaidi kuwahi kutokea. Siamini kuwa karibu naelekea hospitalini kupokea bando langu la furaha. Tarehe ya kujifungua imepangwa !!!," Diana Marua aliandika.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akienda kununua vitu vya mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.

Mama huyo wa watoto wawili alieleza hamu yake kubwa ya kukutana na mtoto wake wa tatu. Hata hivyo alidokeza kuwa hayuko tayari kwa mchakato wa kujifungua.

"Lakini kusema kweli mimi siko tayari kwa thieta, ni jinsi ninavyotazamia kukutana na mtoto inanipa nguvu. Hebu tufanye hivi," Alisema.

Katika chapisho la hapo awali, mke huyo wa Bahati alidokeza kuwa zimesalia wiki chache tu ajifungue.

Katika barua ndefu aliyoiandikia Mungu, Diana aliweka wazi kwamba anafurahi sana kupata nafasi ya kuitwa mama tena.

"Mungu Mpendwa, ASANTE 😭🙏

Ni wewe tu uliyeuelewa moyo wangu nilipohisi kama niko na mimba. Ni wewe tu ulielewa kuchanganyikiwa kwangu, nilihisi kupotea. Ni wewe tu uliyejua vita iliyokuwa akilini mwangu. Niliogopa kurudi kwenye safari hii. Umenifariji.

Nilipochunguzwa mara ya kwanza na kujua Tarehe yangu ya Kujifungua, Kila kitu kiliendana, ilikuwa muujiza, ulizungumza nami 😭 Ukiwa umezungukwa na marafiki na wapendwa, ukimya bado ulikuwa mkubwa sana. Kila kitu kilibadilika niliposikia mapigo ya moyo ya Malaika wangu kwa mara ya kwanza, nilipenda tena. Nililia, nilicheka, nilizidiwa shukrani," Aliandika.

Pia alitumia fursa hiyo kumhakikishia mwanawe ambaye hajazaliwa kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Umebarikiwa sana kuwa na Mama, baba na Ndugu wenye upendo wanaosubiri kukukumbatia na kukupa busu zisizo na mwisho. TUNAKUPENDA," Alimwambia mwanawe.

Diana na Bahati walitangaza ujauzito wa mtoto wao wa tatu pamoja mwezi Julai kupitia wimbo "Nakumbolov."