"Sikufurahia ndoa!" Ben Pol afunguka mazito kuhusu ndoa yake na Anerlisa Muigai iliyovunjika

Wawili hao walitengana mapema mwaka wa 2021.

Muhtasari

•Ben alisema ndoa yao ya miaka mitatu ilihusu sana kujionyesha mitandaoni badala ya kufurahia manufaa halisi ya ndoa.

•Alidokeza kuwa anahisi huenda alitumiwa na mke huyo wake wa zamani kutimiza malengo yake maishani.

•Alikiri kuwa alikuwa amewekeza hisia na mapenzi yake yote kwa kipusa huyo kabla ya mambo kuenda mrama.

Ben Pol na Anerlisa Muigai
Image: HISANI

Staa wa Bongo Ben Pol amekiri kwamba hakuwafurahia ndoa yake ya miaka mitatu na mridhi wa Keroche, Anerlisa Muigai.

Ben Pol alijitosa kwenye mahusiano na binti huyo wa seneta wa Nakuru Tabitha Karanja mwaka wa 2018 kabla ya kufunga pingu za maisha naye mwezi Mei 2020. Wawili hao walitengana mwezi Februari mwaka  wa 2021.

Wakati akizungumza kwenye mahojiano na mtangazaji Millard Ayo, mwanamuziki huyo alisema kwamba ndoa yao ya miaka mitatu ilihusu sana kujionyesha mitandaoni badala ya kufurahia manufaa halisi ya ndoa.

"Kusema kweli nisiwe muongo, ukitoa picha za Instagram na nini, sijaenjoy sana ndoa. Ile mipango ya ndoa, tutengeneze watoto tuzae na nini, sijawahi kuona. Sikuona ndoa kama ninavyoona na watu wengine," alisema.

Mwanamuziki huyo hata hivyo alikiri kwamba alipata pesa nyingi zaidi wakati wa ndoa yake na mrithi huyo wa Keroche.

Hata hivyo, alidokeza kuwa anahisi huenda alitumiwa na mke huyo wake wa zamani kutimiza malengo yake maishani.

"Naona kama niliingia kwenye picha ili kuleta ule ukamilifu!" alisema.

Mwimbaji huyo wa Bongo RnB alibainisha kuwa uhusiano wake na Anerlisa ulikuwa wa kwanza  kabisa wa kweli kuwahi kutokea katika maisha yake na hivyo alikuwa na matumaini makubwa ya ndoa nzuri.

Alikiri kuwa alikuwa amewekeza hisia na mapenzi yake yote kwa kipusa huyo kabla ya mambo kuenda mrama.

"Kiwango cha upendo, kiwango cha kujitolea na kiwango cha kujitoa ambacho nilikuwa nimetoa kwake haijawahi kutokea hapo awali. Sijahi kumpenda mtu mwingine kabla yake. Yalikuwa mahusiano ya kwanza kuzama kabisa na nilikuwa sawa," alisema.

Ben Pol aliweka wazi kwamba ndoa yao haikuvunjika kwa sababu ya masuala ya ukosefu wa uaminifu kwa kila mmoja.

Licha ya kutengana kwao takriban miaka miwili iliyotokea na yote yaliyotokea baina yao, hana kinyongo chochote dhidi yake. Pia alidokeza kwamba bado ana hisia za mapenzi kwa Anerlisa ndani ya moyo wake.

"Tunazungumza.Tulichat kwenye WhatsApp mwezi Juni. Kulikuwa na vitu vyake huku, nilikuwa naenda Nairobi, nikawa naenda kumpatia. Lakini sikuendea mwenyewe, nilimwagiza mtu ampelekee lakini tulikuwa tunazungumza tu," alisema.

Aidha, Ben Pol alibainisha kuwa ingawa ndoa yao haikufanikiwa, mke huyo wake wa zamani ana haki ya kupendwa na mwingine.