"Sikuwa na akili!" Nabii Victor Kanyari afichua ukweli kwa nini alikuwa akidai mbegu ya 310

Mtumishi huyo wa Mungu mwenye utata alifichua kwamba alitumia hila hiyo ili kuepuka umaskini.

Muhtasari

•Kanyari amekiri madai yake ya shilingi 310 kutoka kwa waumini kwa ajili ya maombi na uponyaji katika siku za nyuma hayakuwa ya kweli.

•Kanyari alisema kuwa hata hivyo Mungu alimuelekeza kutoka katika njia aliyokuwa amepitia ya kudai pesa

Pastor Kanyari
Pastor Kanyari
Image: HISANI

Nabii wa Kenya aliyezingirwa na utata mwingi, Victor Kanyari amekiri kwamba madai yake ya shilingi 310 kutoka kwa waumini wake kwa ajili ya maombi na uponyaji katika siku za nyuma hayakuwa ya kweli.

Wakati akiwahutubia waumini wa kanisa lake katika ibada ya hivi majuzi, mtumishi huyo wa Mungu alifichua kwamba alitumia hila hiyo ili kuepuka umaskini.

Alisema kamwe haikuwa nia yake kuwaambia waumini wapande mbegu kwa Sh310 bali ni umaskini ndio ulikuwa umemsukuma hadi kona.

“Si kutaka kwangu, umaskini ulikuwa umenitandika sawasawa lakini nilikuwa na annointing. Ni umaskini,” Nabii Kanyari alisema.

Aliongeza, “Nilianza kuitisha 310 rafiki yangu, lakini sikujua Mungu nipatie akili na maarifa. Pesa nitajitafutia. Mungu alinipa annointing, lakini haikuwa annointing ya pesa. Ilikuwa annointing ya kuponya magonjwa; HIV, nini.. watu walikuwa wanajaa, watu kama elfu kumi. Lakini ile pesa ninapata hainitoshelezi, ni kidogo. Nikaanza mpaka kuitisha 310, nasema panda mbegu. Watu wanatuma.

Kanyari alisema kuwa hata hivyo Mungu alimuelekeza kutoka katika njia aliyokuwa amepitia ya kudai pesa na kumrudisha kwenye njia yake halisi.

“Nilikuwa naitisha 310, watu wanapona. Lakini naenda kwa nyumba, nalala njaa. Sikuwa na chakula. Na nimekuwa nafanya miujiza.

Ilikuwa mpaka Mungu akampa ufunuo ambapo baadaye aliomba apewe hekima na akili ili aweze kutekeleza kazi yake na pia kupata pesa.

“Kutoka siku hiyo, Mungu hakuwahi funga hii huduma tena. Sikuwa kukosa pesa tena. Sasa niko na magari hata nakosa kwa kupeleka. Watoto wanasoma vizuri. Sasa ni wakati wa kusimama na matumizi tu tukisema njoo jinsi Mungu anafanya,” alisema.

Miaka kadhaa nyuma, mtumishi huyo wa Mungu ambaye amekuwa akihubiri kwa miongo miwili iliyopita alizua utata nchini na kote barani baada ya kusambaa mitandaoni kwa kuwataka waandamanaji kumtumia Ksh 310 badala ya maombi maalum na miujiza.