"Sio chungu sana" Jimal Rohosafi aelezea jinsi utaratibu wa upandikizaji wa nywele zake ulifanyika (+video)

"Upandikizaji wa nywele ni kuondolewa kwa nywele kutoka kwa mwili wako hadi eneo unalopenda," alieleza Jimal.

Muhtasari

•Jimal alieleza kuwa utaratibu huo unahusisha kuondolewa kwa nywele kutoka sehemu fulani za mwili wa mtu hadi maeneo ambayo mtu angependelea zaidi.

•Alieleza kuwa yeye binafsi alichagua kuondolewa nywele kutoka nyuma ya kichwa chake na kusogezwa kwenye sehemu ya mbele ya kichwa.

Image: INSTAGRAM// JIMAL ROHOSAFI

Mfanyibiashara maarufu wa Kenya Jimal Marlow Rohosafi amejitokeza kuwaeleza wafuasi wake jinsi utaratibu wa upandikizaji wa nywele unavyofanywa.

Siku ya Jumanne, Jimal ambaye kwa sasa yuko nchini Uturuki kwa ajili ya sehemu ya pili ya upandikizaji wa nywele zake alifichua kwamba amekuwa akipokea jumbe nyingi kutoka kwa watu kutoka kote ulimwenguni ambao hawaelewi jinsi utaratibu huo unafanywa.

Kufuatia hilo, alieleza kuwa utaratibu huo unahusisha kuondolewa kwa nywele kutoka sehemu fulani za mwili wa mtu hadi maeneo ambayo mtu angependelea zaidi.

"Watu wengi hawaelewi upandikizaji wa nywele, napata DM nyingi kutoka kote. Upandikizaji wa nywele ni kuondolewa kwa nywele kutoka kwa mwili wako hadi eneo unalopenda,” Jimal alieleza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mfanyibiashara huyo wa Matatu aliambatanisha maelezo hayo na picha zake akifanyiwa utaratibu huo katika Hospitali ya Uturuki na kueleza kuwa yeye binafsi alichagua kuondolewa nywele kutoka nyuma ya kichwa chake na kusogezwa kwenye sehemu ya mbele ya kichwa.

"Yangu ilitolewa kutoka upande wa nyuma wa kichwa changu ambapo kulikuwa na mengi hadi paji la uso. Baada ya siku chache sehemu iliyoondolewa itakua tena moja kwa moja (siyo chungu sana)," alifichua.

Katika taarifa ya hapo awali, Jimal alidokeza kuwa tamanio la kubaki kijana milele ndiyo sababu inayompa shinikizo la kuenda nchini Uturuki kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa nywele zake.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, baba huyo wa watoto watatu alionyesha video ya mhudumu wa hospitali akimhudumia.

Chini ya video hiyo, alisema kuwa ni ndoto ya kila mtu kutozeeka.

"Ndoto ya binadamu wote ni kukaa mchanga milele," Jimal aliandika chini ya video aliyopakia kwenye mtandao wa Instagram.

Aliambatanisha video hiyo na wimbo wa ‘Young Forever’ wa Jay-Z na Mr Hudson.

Katika chapisho lingine, mfanyabiashara huyo wa matatu alibainisha kuwa kupandikiza nywele ni njia ya kujionyesha upendo.

"Daima jipende mwenyewe kwanza," aliandika chini ya picha ya kichwa chake ambayo alichapisha.

Jimal pia amefichua kuwa mbali na utaratibu wa kupandikiza nywele pia ana mpango wa kufanyiwa utaratibu maalum wa kupunguza uzito wa mwili wake.

"Ninahitaji kupungua kutoka kilo 95 hadi 75 katika miezi 4. Leo ni Allurion Intragastric Balloon: Hatua kwa hatua,” aliandika.