"Sio rahisi!" Huddah Monroe afichua kwa nini bado hajaolewa licha ya kuwa mrembo sana

Mwanasosholaiti huyo mrembo kwa muda mrefu amekuwa msiri sana kuhusu mahusiano yake.

Muhtasari

•Mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 31 alidokeza kuwa ndoa si ndoto yake akiashiria kuwa si jambo rahisi.

•Huddah alifichua kuwa hata angechukua hatua ya kuingia kwenye ndoa, angeiweka faragha mbali na macho ya umma.

Huddah Monroe
Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mwanasosholaiti maarufu Huddah Monroe aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram ambapo alijibu baadhi ya maswali kuhusu maisha yake.

Moja ya maswali muhimu aliyoulizwa ni kwa nini bado hajapata mwanaume wa kumuoa rasmi licha ya urembo wake wa kuvutia.

“Mbona mpaka leo hujaoleka wakati wewe ni mrembo?,” mtumizi wa Instagram alimuuliza.

Katika majibu yake, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 31 alidokeza kuwa ndoa si ndoto yake akiashiria kuwa si jambo rahisi.

Wakati huohuo, alifichua kwamba hata ikiwa angechukua hatua ya kuingia kwenye ndoa, angeiweka faragha mbali na macho ya umma.

“Umeshawahi kujiuliza si ndoto ya kila mtu. Ndoa sio matembezi kwenye bustani (si rahisi). Ni ngumu kuliko unavyofikiria. Na kama ningeolewa usingejua. Hilo litakuwa la faragha milele,” Huddah Monroe alisema.

Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mrembo huyo wa Kenya ambaye wakati mwingine anaishi Dubai kwa muda mrefu amekuwa msiri kuhusu mahusiano yake.

Mwaka uliopita, Huddah alidaiwa kutoka kimapenzi na mwimbaji wa Tanzania Juma Jux baada ya wawili hao kuonekana wakiwa pamoja mara kadhaa. Wawili hao hata hivyo baadaye walijitokeza kuweka wazi kuwa hakuna mahaba kati yao na kudai kwamba uhusiano wao ni wa kirafiki na kibiashara tu.

Katika kipindi cha Maswali na Majibu mwezi Septemba, Mwanasosholaiti huyo alifichua kuwa 'mahusiano' yake na Jux yalikuwa ni mradi tu ambao walikuwa nao pamoja na tayari ulikuwa umeisha kufikia mwezi huo.

"Kama Raila, Ulikuwa tuu mradi. Na uliisha," Huddah alisema kwenye Instagram.

Hapo awali, wawili hao waliwakanganya mashabiki wao kuhusu uhusiano wao halisi baada ya kuonekana pamoja mara kwa mara na hata kufanya mambo mbalimbali ambayo yalidokeza wanachumbiana. Wawili hao walionekana wakijivinjari pamoja, wakikumbatiana na hata kupigana busu hadharani.

Katika video moja ambayo iliwaonyesha wakiwa wamebarizi nyumbani kwake Juma Jux, wawili hao hawakuogopa kubusu midomoni mbele ya kamera na kuambiana maneno matamu matamu ya kimapenzi. 

"Mimi na mpenzi wangu tumetulia tu.. sijui, ningependa kuwa kitandani na wewe," Huddah alisikika akimwambia Jux.