Sipo kwenye ndoa! Dadake Diamond, Queen Darleen afunguka sababu za kumtema mumewe

Darleen alisema aliamua kuchagua ustawi wa mtoto wake badala ya ndoa yake.

Muhtasari

•Darleen alipuuzilia mbali madai kuwa aligura ndoa yake baada ya kuwa na uhusiano mbaya na mke mwenza.

•Hali halisi ya ndoa ya Darleen inatatanisha kwani anadai kuwa hajui kuhusu msimamo wa mumewe Isihaka.

Queen Darleen na mumewe Isihaka
Queen Darleen na mumewe Isihaka
Image: HISANI

Siku ya Jumatano, dadake Diamond Platnumz, Queen Darleen alitangaza uamuzi wake wa kugura ndoa yake na Bw Isihahaka Mtoro.

Msanii huyo wa WCB alisema kwamba aliamua kuchagua ustawi wa mtoto wake badala ya ndoa yake.

"Nimekubali kumuacha mtu ninayempenda ili kumlinda mtu ninae mpenzi zaidi. Nampenda sana mwanangu. Balqis Isihaka Mtoro🙌🙌🙌🙌 Wakubwa wenzangu mtanielewa," Queen Darleen alitangaza kupitia Instagram.

Katika mahojiano ya kufuatilia na Wasafi Media, mama huyo wa mtoto mmoja alisisitiza kuwa kwa sasa hayupo kwenye ndoa.

Hali halisi ya ndoa ya Darleen hata hivyo inatatanisha kwani alidai kuwa hajui kuhusu msimamo wa mumewe Isihaka na ambaye ni baba ya mtoto wake.

"Kwa mimi, nafsi yangu naweza kusema sipo kwenye ndoa. Kwa yeye sijui. Mimi sipo kwenye ndoa! Lakini mume wangu Isihaka yupo, anamlea mtoto, lakini mimi siko kwenye ndoa," Darleen alisema.

Binti huyo wa Mzee Abdul alidai kuwa mumewe pekee ndiye anayeweza kueleza msimamo wake kwa ndoa yao.

Darleen alidokeza kuwa ndoa yake ilianza kuyumba muda mrefu uliopita. Hata hivyo alikiri kuwa bado ana mapenzi makubwa kwa Bw Isihaka.

"Nampenda kufa. Ndio maana kuna kipindi mliona nimekonda mkanisema sana. Nilikuwa napambana na hali ya kusema kuwa sipo kwenye ndoa," Alieleza Darleen.

Dada huyo wa Diamond alipuuzilia mbali madai kuwa aligura ndoa yake baada ya kutoelewana na mke mwenza wake.

Pia aliweka wazi kuwa ingawa anafahamu fika kuwa mumewe ana mke mwingine hajawahi kukutana wala kukabiliana naye.

"Mimi niko pekee yangu, sina mke mwenza kwa aliyekuwa mume wangu au mume wangu. Huyo ni mtu ambaye sikuwahi kuonana naye. Ananiona kwenye mitandao, mimi simuoni. Sijawahi kucheza nyae. Sio shoga wangu," Alisema.

Darleen pia alibainisha kuwa kamwe hajawahi kumfumania mumewe ama kupata meseji za mapenzi kwenye simu yake.

Mwanamuziki huyo alisema ataweka sababu zote zilizopelekea hali hiyo wakati mumewe atampatia ruhusa. Alisema kwa upande wake uhusiano wao wa sasa umebaki ni wa kulea mtoto tu.