Tanasha Donna afunguka kwa nini hangependa mwanawe kuwa msanii kama yeye na Diamond

Tanasha hata hivyo alidokeza kuwa kuna uwezekano wa mwanawe kufuata nyayo zake na Diamond.

Muhtasari

•Tanasha alisema kuwa katika siku za usoni angependa mwanawe ajihusishe na michezo kama vile soka badala ya muziki.

•Tanasha alibainisha kuwa kimsingi, wanamichezo huwa na nidhamu sana tofauti na wanamuziki.

Tanasha na mwanawe Naseeb Junior
Image: Tanasha Donna/INSTAGRAM

Mwimbaji na mwanamitindo maarufu wa Kenya Tanasha Donna ameweka wazi kuwa matamanio yake ni mwanawe kuwa mwanaspoti.

Katika mahojiano na Mpasho, Tanasha alisema hangependa mwanawe Naseeb Juniour awe mwananamuziki kama yeye na mzazi mwenzake Diamond Platnumz.

Alieleza kuwa katika siku za usoni angependa sana mtoto huyo wake wa pekee ajihusishe na michezo kama vile soka badala ya muziki.

"Nahisi kama kuna uwezekano. Mama yake ni mwimbaji na baba yake ni mwimbaji. Kuna uwezekano mkubwa wa yeye kufuata njia hiyo, Mungu pekee ndiye ajuaye. Ingekuwa kwa matakwa yangu, ningemtaka awe mwanasoka," Tanasha alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond alibainisha kuwa kimsingi, wanamichezo huwa na nidhamu sana tofauti na wanamuziki.

"Najua watu wanaojihusisha na michezo wana nidhamu sana. Wanaamka mapema, wanafanya mazoezi, wanakimbia, hawanywi pombe kwa sababu kuna vipimo vinavyofanywa kila wakati. Ingekuwa juu yangu, ningetaka hivyo kwa sababu tasnia hii ya muziki inakuja na mengi. Kuna siasa nyingi nyuma yake," Alisema.

Aliongeza "Kuna mengi ambayo huendelea katika tasnia ya muziki. Ukiwa una ushawishi na uko na pesa nyingi, unaweza kuendesha mambo mengi. Ndivyo hukuwa kwenye tasnia nyingi. Hata hivyo naamini kila tasnia huja na mazuri yake na mabaya yake. Hata michezo huwa na upande wake mbaya," 

Tanasha hata hivyo alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mwanawe huyo kufuata nyayo zake na Diamond.

Aliweka wazi kuwa ikitokea Naseeb awe mwanamuziki basi hatasita kuunga mkono taaluma yake na kumsaidia kuikuza.

"Lakini ikitokea afanye muziki nitamuunga mkono kikamilifu na nitakuwa na uzoefu wa kumwelekeza katika njia sahihi. Acha tuone, muda utasema," Alisema.

Hivi majuzi wakati Tanasha alikuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa, Naseeb Juniour alitengeneza video akimsherehekea.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka miwili alirekodi wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa mama yake kwa sauti nzuri.

Naseeb ni mtoto wa pekee wa Tanasha na mzaliwa wa nne wa staa wa Bongo Diamond Platnumz.