Tanasha Donna na aliyekuwa mpenziwe Diamond watofautiana kuhusu ndoa

Diamond na Tanasha walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi cha takriban miaka miwili.

Muhtasari

•Tanasha Donna alisema kuwa  anaamini kwamba ndoa haipaswi kubadili mtazamo wa mtu kwenye kazi.

•Diamond aliweka wazi kuwa hana haraka ya kujitosa kwenye ndoa huku akidai kwamba huwa inapunguza kasi ya kazi.

katika picha ya maktaba
Tanasha Donna na Diamond katika picha ya maktaba
Image: HISANI

Msanii na mwanamitindo wa  Kenya Tanasha Donna ametofautiana na kauli za aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz kuwa ndoa inapunguza kasi ya kazi.

Katika mahojiano na Mpasho, Donna alisema anaamini kwamba ndoa haipaswi kubadili mtazamo wa mtu kwenye kazi.

Alisema kuwa wanandoa bado wanaweza kutimiza malengo yao hata baada ya kufunga pingu za maisha.

"Naamini kuwa mnaweza kuwa kwenye ndoa na nyote wawili mtimize ndoto zenu. Sioni tatizo lolote na hilo. Sidhani eti nkifunga ndoa lazima mambo yote yabadilike na kufanya nisiangazie ndoto zangu tena eti kwa sababu lazima niangazie kusimamia kwangu. Inategemea na wanadoa," Alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja aliweka wazi kuwa hakubaliani na mtazamo wa jamii kuhusu ndoa. Alisema ndoa sio ya wanandoa pekee ila pia Mungu huwepo.

"Ndoa sio yenu pekee, ni ya Mungu pia. Ukiangalia, watu hukula kiapo mbele ya Mungu na kuapa kuwa pamoja mpaka kifo," Alisema.

Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya Diamond ambaye ni baba wa mwanawe kudokeza kwa nini anahofia ndoa.

Staa huyo wa Bongo aliweka wazi kuwa hana haraka ya kujitosa kwenye ndoa huku akidai  kuwa hatua hiyo huwa chanzo cha mwisho wa taaluma za wengi.

"Mimi tayari nimeshatulia. Lakini kwa ndoa, unajua mimi bado nataka kuwapa muziki kwa sana, mimi chenye nimeona ni kwamba nikioa mwanamke basi atanitoa kwenye njia yangu ya kufanya muziki na kuvuruga azma yangu ya kufanya muziki zaidi,

Alifichua kuwa aliogopa ndoa baada ya kuona  taaluma za baadhi ya rafiki yake zikifeli mara tu baada ya kuoa.

"Nimeliona hilo kutoka kwa rafiki zangu wote. Kwa sasa wacha niwape muziki na ikifika muda nimekaribia kustaafu basi nitaoa,” Diamond alisema.

Diamond na Tanasha walikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi cha takriban miaka miwili.

Walichumbiana kati ya 2018 na 2020 na kubarikiwa na mtoto mmoja pamoja, Naseeb Juniour, mnamo Oktoba 2019.