Tayari kurudi soko? Harmonize afanya vipimo vya UKIMWI baada ya kuachwa na Kajala

Harmonize alichukua hatua ya ujasiri ya kufanyiwa vipimo vya UKIMWI.

Muhtasari

•Harmonize alichapisha matokeo ya hali yake ya VVU kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya kufanya vipimo.

•Harmonize alifanya vipimo hivyo katika kipindi ambapo inaaminika kuwa yuko singo baada ya kuachwa na Kajala.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Siku ya Jumanne, bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize  alichukua hatua ya ujasiri ya kufanyiwa vipimo vya UKIMWI.

Harmonize alichapisha matokeo ya hali yake ya VVU kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya kufanya vipimo.

"Imekamilika✔🙏🙏🙏" aliandika chini ya kifaa cha kupimia VVU ambacho kilionyesha kuwa hana virusi hivyo.

Staa huyo wa Bongo pia alionyesha ushahidi wa video wa kipimo hicho ili kudhibitisha kuwa yuko salama kwa virusi hivyo.

"Waoga ndio tunakaaga ivi vitu ndani," alisema kabla ya kupimwa.

Harmonize alifanya vipimo hivyo katika kipindi ambapo inaaminika kuwa yuko singo baada ya kuachwa na mchumba wake Kajala Masanja.

Wiki jana, muigizaji huyo alidokeza kutengana kwao kufuatia shinikizo kubwa la mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwataka kuvunja ukimya na  kuweka wazi hali ya mahusiano yao ya miezi michache.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema kupitia Instagram.

"Hakika nimekosea familia yangu, ndugu zangu, na marafiki zangu. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa. Namsemehe X wangu na niko tayari kuenda kwa mwingine." 

Harmonize hata hivyo amesalia kimya kuhusu kutengana na Kajala Masanja licha ya shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wake  wakimtaka aweke wazi yaliyojiri kati yake na muigizaji huyo mkongwe wa Bongo.

Kajala alirejea nyumbani siku ya Jumanne baada ya kudaiwa kuwa kwenye likizo kwa muda. Kumekuwa na madai kwamba muigizaji huyo alienda likizo fupi  ili kutuliza akili baada ya kutengana na Harmonize.