“Tuliachana!” Akothee ajibu vikali baada ya kuulizwa kuhusu harusi ya pili iliyokuwa ifanyike Ulaya

Baada ya harusi yao ya kwanza mwezi Aprili, Akothee alitangaza kuwa wangefanya harusi ya pili nchini Uswizi mwezi Julai.

Muhtasari

•Akothee alisema kwa mzaha kwamba alitengana na mumewe Denis Shweizer mara tu baada ya harusi yao ya kwanza iliyofanyika Aprili 10 mwaka huu.

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alitaka mwanamitandao kuangazia maisha yake mwenyewe na kusonga mbele.

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee alionekana kujawa ghadhabu baada ya kuulizwa kuhusu mipango ya harusi yake ya pili na mumewe mzungu Denis 'Omosh' Shweizer ambayo iliratibiwa kufanyika Uswizi.

Chini ya moja ya machapisho yake, shabiki alimuuliza kuhusu mipango ya harusi hiyo ambayo awali alikuwa ametangaza kuwa ingefanyika Julai.

“Madam Boss hatujasahau ile harusi yako kubwa ya majuu, kwani ni lini,” mtumizi mmoja wa mtandao wa Instagram alimuuliza Akothee.

Katika jibu lake, mama huyo wa watoto watano alisema kwa mzaha kwamba alitengana na mume wake Denis Shweizer mara tu baada ya harusi yao ya kwanza iliyofanyika jijini Nairobi mnamo Aprili 10 mwaka huu.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alitaka mwanamitandao kuangazia maisha yake mwenyewe na kusonga mbele.

"Tuliachana tarehe 11 Aprili, sasa chukua maisha yako na uendelee," alijibu.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Baada ya harusi yao ya kwanza mwezi Aprili, Akothee alitangaza kuwa wangefanya harusi ya pili nchini Uswizi Julai, mwezi uliopita.

Katika tangazo lake, Akothee alisema angepeleka kikosi chake kizima cha wapambe hadi  Uswizi kwa sehemu ya pili ya harusi.

Wakati huo, mama huyo wa watoto watano alifichua majina 17 ya watu ambao wangepamba hafla hiyo ya pili wakiwemo mabinti zake watatu; Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia. Wengine ni pamoja na mbunge  wa Lang'ata Jalang'o, Kabi na Milly Wajesus, Azziad Nasenya,  Mimi, Janet Otieno, Nina Ajigo, Fiona Morema, Lulu, Mokeira Onchiri, Evander Holyfield, Beatrice Schnelli Okello na Geret.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya harusi ya Aprili, baada ya kumlaki nchini bintiye Fancy Makadia, Akothee aliweka wazi kuwa wanawe wawili wanaoishi Ufaransa, Prince Ojwang na Prince Oyoo hawakuweza kufika kwenye harusi ya Aprili 10 kwa sababu ya sheria za shule yao lakini akadokeza kwamba wawili hao wangeshuhudia sherehe ya pili iliyoratibiwa kufanyika Uswizi mnamo Julai 10.

"Karibu Prudence Vanpelt, bintiye Akothee. Msilete propaganda na siasa za familia kwa harusi yangu. Watu pekee ambao watakosa harusi yangu ni wanangu wawili ambao hawatafanikiwa kwa sababu ya sheria za shule, lakini watashuhudia ambayo imeratibiwa kufanyika Julai 10. Mwaka mzima Akothee anaolewa," alisema.