"Tunashikwa lini?" Karen Nyamu ajibu kwa kejeli maoni kuhusu kuiba mume wa wenyewe

Seneta huyo pia alijibu kwa kejeli baada ya kuitwa "M-kopo mfuliza wa Thamweli."

Muhtasari

•Mtumiaji wa Facebook alimweleza seneta Nyamu kwamba wezi wa mume wa mwingine ni sawa na wezi wa benki.

•Nyamu hajawahi kuogopa kutetea uhusiano wake na mwimbaji huyo wa Mugithi hadharani licha ya kukabiliwa na ukosoaji mwingi.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta mashuhuri wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu kwa muda mrefu amekuwa akikosolewa vikali kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Karen Nyamu na Samidoh wamekuwa wakichumbiana kwa miaka kadhaa sasa na wawili hao wamejaliwa kupata watoto wawili pamoja. Licha ya wao kuonyesha hadharani kwamba wana furaha kuwa pamoja, ni dhahiri kwamba si kila mtu anafurahia uhusiano wao.

Wapenzi hao wamekuwa wakikosolewa vikali na wakosoaji wao huku seneta huyo wa UDA mara nyingi akishutumiwa kwa kuiba mume wa mtu mwingine.

Ni kisa sawa na tukio la hivi majuzi ambapo chini ya moja ya machapisho, mtumiaji wa Facebook kwa jina Ptah Petta Peesh alimweleza kwamba wezi wa mume wa mwingine ni sawa na wezi wa benki.

“Btw pastor alisema hakuna mwizi wa bwana na benki. Wote ni wezi,” Ptah alitoa maoni.

Katika jibu lake, seneta Nyamu aliuliza kwa kejeli, “Sisi tunashikwa lini.”

Mtumiaji mwingine wa mtandao wa Facebook kwa kejeli alimuita "M-kopo mfuliza wa Thamweli." Akimaanisha M-kopo na Fuliza ya Samidoh.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na drama nyingi alijibu kwa ujasiri, "Bora tu ni wake."

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Bi Nyamu hajawahi kuogopa kutetea uhusiano wake na mwimbaji huyo wa Mugithi hadharani licha ya kukabiliwa na ukosoaji mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu jambo hilo.

Hivi majuzi, mwanasiasa huyo alibainisha kuwa ni kitendo cha Mwenyezi Mungu kuwa Samidoh alimchukua kuwa mpenzi wake huku akibainisha kwamba alikuwa akiomba kila mara watoto wake kuwa na baba yao.

Alifichua kwamba katika sala zake, kila mara alimwomba Mungu ashughulikie hali iliyoikumba familia yake na mambo yaende sawa.

“Mungu hufanya kazi kwa njia zisizoeleweka. Mimi kuna vile nilikuwa naomba naambia Mungu namwambia ‘ulinipa watoto wazuri, baba yao anawapenda. Ana watoto wengine ambao anawapenda sana, ana mwanamke mwingine ambaye anampenda sana...’

Siku zote nilimwomba Mungu ashughulikie hali hiyo. Nilimlilia kutoka moyoni mwangu. Labda yule mwanamke mwingine naye alilia kwa Mungu kutoka moyoni mwake. Nasema ogopa Mungu. Mungu hupanga mambo yake. Tunatumai matokeo bora tu. Tunatumai mambo yatafanikiwa kwa pande zote mbili. Hatujakata tamaa kwa upande huo mwingine. Bado tunaomba mambo yafanyike,” alisema.

Bi Nyamu amewahi kupuuzilia mbali madai ya kuiba mume wa wenyewe mara nyingi katika siku za nyuma.