"Ulinitambulisha mbinguni hapa duniani" Grand P amsherehekea mpenzi wake Eudoxie Yao

Muhtasari

•Grand P alisema ujio wa Yao katika maisha yake ulimfanya ajihisi kama yupo mbinguni angali duniani.

•Yao aliwasherehekea mashabiki wake huku akiwahakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwao.

Image: FACEBOOK// GRAND P

Mwanasoshalaiti mashuhuri kutoka Ivory Coast Eudoxie Yao aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Jumanne.

Kipusa huyo aliyebarikiwa na umbo unaowaacha wanaume wengi wakidondokwa na mate alitumia fursa hiyo kumshukuru Mola kwa hatua ambazo amepiga maishani kufikia saa.

Pia aliwasherehekea mashabiki wake huku akiwahakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwao.

"Leo ni siku maalum kwangu. Malkia wa Juni 14. Namshukuru MUNGU kwa baraka hizi zote maishani mwangu. Asante Mungu kwa kunipa mwaka mmoja zaidi. Leo ndio siku yangu wapenzi wangu . Njooni mnibariki kidogo itanifanyia mema. Nawapenda sana, maisha marefu yenye afya tele kwenu nyote," Yao alisema kupitia Facebook.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha zake kadhaa zenye mng'ato, huenda kama njia ya kujigamba kuhusu umbo wake.

Mpenzi wake Grand P pia alitumia fursa hiyo kumsherehekea na kumshukuru kwa kuwa chanzo cha furaha yake.

Bilionea huyo mbilikimo alisema ujio wa Yao katika maisha yake ulimfanya ajihisi kama yupo mbinguni angali duniani.

"Maneno hayawezi kuelezea jinsi ninavyohisi juu yako. Kwa kuja maishani mwangu, ulinitambulisha mbinguni duniani. Kutoka chini ya moyo wangu leo ​​napenda tu kukushukuru kwa furaha yote unayoniletea.. Kheri za siku ya kuzaliwa mpenzi wangu. Mola alinde penzi letu," Grand P alimwambia mpenziwe kupitia Facebook.

Yao hata hivyo alieleza ghadabu yake kutokana na kuchelewa kwa mwanamuziki huyo kutoka Guinea katika kumtakia kheri za siku ya kuzaliwa.

"Nimekasirika sana kwa sababu saa hii ndio unanitakia kheri za siku ya kuzaliwa," Alijibu chini ya chapisho la Grand P.

Wawili hao ambao wana utofauti mkubwa wa kimaumbile wamekuwa kwenye mahusiano ya misimu kwa kipindi kirefu.

Wana mamilioni ya wafuasi kutoka kote duniani hasa kutokana na maswali mengi yanayoibuka kutokana na mahusiano yao.