Vera afichua jinsi alivyokuja kugundua ni mjamzito miezi minne baadaye

Ilikuwa vigumu kujua ni mjamzito kwani bado alikuwa akimnyonyesha bintiye.

Muhtasari

•Vera alisema kuwa alichukua hatua ya kufanya vipimo vya ujauzito baada ya kuhisi uchovu mkubwa usio wa kawaida.

•Pia alifichua anapanga kujifungua mtoto wake wa pili kwa njia ya upasuaji kama ilivyokuwa na ujauzito wake wa kwanza.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti Vera Sidika amefichua kuwa alikuwa amebeba ujauzito wake kwa miezi mitatu unusu wakati alipofanya vipimo.

Akizungumza baada ya kutangaza ujauzito wa mtoto wake wa pili siku ya Jumatatu, mama huyo wa binti mmoja alisema kuwa alichukua hatua ya kufanya vipimo vya ujauzito baada ya kuhisi uchovu mkubwa usio wa kawaida.

Alieleza kwamba ilikuwa vigumu kwake kushuku ana mimba mapema kwa sababu alikuwa bado akimnyonyesha bintiye Asia Brown.

"Haikuwezekana kujua kwamba mimi ni mjamzito kwa vile sikuwa nikipata hedhi kwani nilikuwa nanyonyesha na huwa sipati dalili zozote za ujauzito hata kidogo. Ikiwa sikupima labda ningejua hadi miezi 5," alisema kupitia Instagram.

Alisema kuwa daktari wake alimshauri akome kumnyonyesha binti yake wakati ujauzito wake ukitimiza miezi minee hadi mitano.

"Sikuwahi kupata dalili za ujauzito nikiwa na ujauzito wa Asia. Sina dalili kabisa za ujauzito huu pia. Kusema kweli ni baraka sana kupata mimba laini. Nimebarikiwa," alisema.

Mwanasoshalaiti huyo pia alifichua kwamba anapanga kujifungua mtoto wake wa pili kwa njia ya upasuaji kama ilivyokuwa na ujauzito wake wa kwanza.

"Ilikuwa laini sana mara ya mwisho. Ilikuwa vizuri. Nitaifanya tena," alisema.

Vera Sidika alitangaza ujauzito wa mtoto wake wa pili na mumewe Brown Mauzo siku ya Jumatatu kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Katika tangazo lake, mama huyo wa binti mmoja alifichua kwamba amekuwa mjamzito kwa takriban miezi saba sasa.

"Wapendwa, ndugu wa Asia yuko njiani!!!🎊💃🏼Mungu alikuwa na mipango ya familia yetu ndogo kukua zaidi 🙏  Tuliegundua tukiwa na miezi 4 na nusu," alisema.

Vera aliambatanisha ujumbe huo wake na picha inayomuonyesha akiwa ameshikilia tumbo lake kubwa lililochomoza.

Alifichua alikuwa akipanga kuenda nje ya nchi ili kufanyiwa upasuaji wa kuongeza matiti wakati alipogundua kuwa ni mjamzito.

"Ilinibidi kufuta safari yangu na kukumbatia muujiza wetu mdogo 😍🎊Nimejifunza kwamba kuwa mjamzito inamaanisha kuwa kila siku ni siku nyingine karibu na kukutana na mpenzi mwingine wa maisha yetu," alisema.

Kufuatia hilo, mwanasoshalaiti huyo alitoa shukrani za dhati kwa mumewe kwa kufanikisha ujauzito wa pili.

Aidha, alieleza furaha yake kubwa kuona kuwa bintiye mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili atapata ndugu hivi karibuni.

"Nimefurahi sana kwamba Asia anapata ndugu ambaye atakua naye. BFF inapakia 💃🏼,"