(+Video) Baby Mama wa Bahati, Yvette Obura adokeza mahusiano mapya

Muhtasari

•Yvette Obura amedokeza kuwa amezama tena kwenye dimbwi la mahaba baada ya kukaa kipindi kirefu bila kuwa kwenye mahusiano.

•Haya yanajiri takriban mwaka mmoja baada ya malkia huyo kutengana na mpenzi wake wa hivi majuzi Trevor Nzomo.

Image: INSTAGRAM// YVETTE OBURA

Aliyekuwa mpenzi wa Bahati, Yvette Obura amedokeza kuwa amezama tena kwenye dimbwi la mahaba baada ya kukaa kipindi kirefu bila kuwa kwenye mahusiano.

Hii ni kutokana na video aliyopakia Instagram ambayo inaonyesha matukio ya likizo aliyoenda wikendi na  mwanamume ambaye amemtaja kama "Bestfriend."

Video hiyo inaonyesha mama huyo wa binti mmoja akiwa likizoni katika hoteli ya kifahari na mwanaume huyo aliyefichwa sura.

"Nilipumzika kutoka kwa kawaida wikendi hii na kwenda likizo na bestfriend yangu. Shukran kwa @urbanvacations kwa kupanga likizo nzuri hivi. Tulipenda kila kitu," Yvette aliandika chini ya video ambayo alipakia.

Kwenye video hiyo, Yvette anaonekana akiwa ameshika mkono wa kushoto wa mwanaume huyo  na kuacha atumie mkono wa kulia kuendesha gari.

Baadae wawili hao wanawasili hotelini na kuelekea kwa chumba kilichopambwa kwa maua mekundu kila mahali.

Maua hayo pia yalikuwa yametumika kuchonga maandishi "Nakupenda sana" juu ya kitanda  kikubwa ndani ya chumba hicho.

Itazame video hiyo hapa:

Haya yanajiri takriban mwaka mmoja baada ya malkia huyo kutengana na mpenzi wake wa hivi majuzi Trevor Nzomo.

Yvette na Bahati walitengana zaidi ya miaka mitano iliyopita baada ya kubarikiwa na mtoto wa kike pamoja.

Baadae mwanamuziki huyo alijitosa kwenye mahusiano na mke wake wa sasa Diana Marua ambaye wana watoto wawili naye.

Hivi majuzi Yvette alifichua kuwa ilimchukua miaka minne kukubali kumsamehe Bahati kufuatia kutengana kwao. 

"Niliacha kila kitu iende, na ilinichukua miaka 3 kuelekea 4 kusahau kila kitu na kuwasemehe."  Yvette alisema kwenye mazungumzo na Diana.

Yvette aliweka wazi kuwa kwa sasa hana kinyongo chochote na Diana na mumewe kwani tayari amesonga mbele na maisha yake.