"Walimdharau sana na kumkebehi!" Ndugu ya Diamond Platnumz awaanika marafiki wake wanafiki

Muhtasari

•Jons amefichua kuwa kuna baadhi ya watu wa karibu ambao walimdharau ndugu yake Diamond Platnumz wakati alikuwa fukara bila mbele wala nyuma.

•Mama Dangote ni miongoni mwa watu ambao wameiunga mkono kauli ya Jons huku akiichapisha tena kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Image: INSTAGRAM// ROMY JONS

Mcheza santuri  Romeo Abdul Jones almaarufu Romy Jons amewashauri watu wapendane na wathaminiane bila kuangazia uwezo wa kifedha wa wenzao.

Jons ametoa kauli hiyo kwenye Instastori zake huku akifichua kuwa kuna baadhi ya watu wa karibu ambao walimdharau ndugu yake Diamond Platnumz wakati alikuwa fukara bila mbele wala nyuma.

Ameeleza kuwa miaka ya hapo awali kuna baadhi ya watu wanaojiita marafiki wa Diamond ambao hawakuwahi kuamini katika ndoto zake.

"Kuna baadhi ya ndugu au marafiki ambao walimdharau sana na kumkebehi mdogo wangu Nasibu. Hakuna aliyeamini katika ndoto zake," Jons alisema.

Jons alifichua kuwa wengi wa waliomkebehi na kumdharau Diamond siku za hapo awali ndio ambao sasa wapo katika mstari wa mbele kuomba msaada.

"Leo ndio hao mstari wa mbele kuomba msaada!!! Tupendane na kuthaminiana hata kama hatuna mbele wala nyuma," Alisema Jons.

Mama Dangote ni miongoni mwa watu ambao wameiunga mkono kauli ya Jons huku akiichapisha tena kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Romy Jons ni binamu wa Diamond ingawa  wawili hao huwa wanajitambulisha kama mandugu. Jons pia ndiye DJ rasmi wa Diamond. 

Diamond ambaye ana umri wa miaka 31 alijitosa kwenye fani ya muziki takriban mwongo mmoja unusu uliopita.

Tangu wakati huo ameendelea kubobea taratibu na sasa anatambulika kote duniani na anamiliki lebo yake, media yake na ameweza kujijengea utajiri mkubwa mno.