"Walipendeza sana!" Msanii wa Harmonize, Ibraah akiri kumiss mahusiano yake na Kajala

Ibraah aliweka wazi kuwa alipendezwa na ndoa ya muda mfupi ya wasanii hao wawili.

Muhtasari

•Ibraah alisema alifurahi sana baada ya bosi wake kurudiana na Kajala na kubainisha kuwa alikuwa na matumaini makubwa na mahusiano yao.

•Ibraah alifichua kuwa Kajala ndiye mpenzi pekee wa bosi wake ambaye aliwahi kuwa na ukaribu naye.

Harmonize, Kajala, Ibraah
Image: HISANI

Staa wa Bongo  Ibrahim Abdallah Nampunga almaarufu Ibraah amekiri kwamba anayamiss mahusiano ya Harmonize na Kajala Masanja.

Akizungumza kwenye mahojiano na Rick Media, Ibraah aliweka wazi kuwa alipendezwa na ndoa ya muda mfupi ya wasanii hao wawili.

Alisema alifurahi sana baada ya bosi wake kurudiana na Kajala na kubainisha kuwa alikuwa na matumaini makubwa na mahusiano yao.

"Niliona kwamba  ni watu ambao wamekusanya shida zao, matatizo yao yote ambayo wamepitia wakaweka kando na kusema kwamba ule ni utoto. Wakasema yale ni mapito ambayo tulipita, tuko sawa tuende tujenge future," Ibraah alisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 24 alisema aliona kana kwamba wawili hao walikuwa wamejikita katika kuzika ya kale na kufanyia kazi uhusiano wao.

 "Nilijua ni watu ambao wanawaza kufanya makubwa zaidi kwenye mahusiano yao, ni watu ambao wanafocus  na mahusiano yao kuangalia wapi wanajenga zaidi na ni mahali walipokosea wameshahau," alisema.

Ibraah alidokeza kuwa alihuzunika wakati uhusiano wao ulipovunjika lakini akaweka wazi kuwa hajui kilichowatenganisha.

"Yamekuja yakatokea, siwezi kusema labda  ni vibaya ama ni vizuri kwa sababu vilivyowakuta vimewakuta wao wenyewe, wao wenyewe ndio wanajua uzito ambao wamepitia na hicho kilichowakuta wakawa tofauti,"

Mwimbaji huyo wa kibao 'Sielewi' alifichua kuwa Kajala ndiye mpenzi pekee wa bosi wake ambaye aliwahi kuwa na ukaribu naye.

Alifichua kuwa alimjua Harmonize alipokuwa akichumbiana na Sarah Michelloti ila hakuwahi kupata nafasi ya kuwa na ukaribu naye.

"Katika mashemeji wangu ambao nimepata muda wa kuongea sana naye, ni yeye (Kajala). Wajua kwangu sio mbali na kwa bro. Wakati mwingine nilikuwa naenda pale tunapiga stori," alisema mwanamuziki huyo.

Ibraah hata hivyo alibainisha kuwa alikuwa akizungumza na Kajala walipokutana ila hawakuwa wanapigiana simu.

"Walikuwa wanapendeza sana!" alisema.

Kajala alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake na Harmonize katikati mwa mwezi Desemba na kusema amesonga mbele na maisha yake.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba tayari amemsamehe mpenzi huyo wake wa zamani kwa aliyofanya.