Mwanamuziki Brian Mutinda almaarufu Brown Mauzo ameibua wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya ndoa yake na Vera Sidika baada ya kufuta picha zote na mwanasosholaiti huyo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Isitoshe, msanii huyo kutoka eneo la Pwani pia ameacha kumfuatilia mzazi huyo mwenzake kwenye mtandao huo. Haijabainika kwa nini alichukua hatua hiyo lakini ni wazi kuwa kuna kitu kinachoendelea kati ya wawili hao.
Upekuzi mdogo kwenye akaunti ya Instagram ya Vera Sidika umebainisha kuwa bado angali anamfuatilia mwimbaji huyo na picha zao bado zilikuwepo kufikia siku ya Jumatatu, Aprili 17 mwendo wa saa tano asubuhi.
Haya yanajiri huku wanandoa hao wakiwa wanatarajia mtoto wao wa pili pamoja. Wawili hao ambao wamekuwa wakichumbiana kwa zaidi ya miaka miwili walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza mwaka wa 2021.
Mwishoni mwa mwaka jana, Vera alifichua atafunga pingu za maisha na mzazi huyo mwenzake mwaka wa 2023 au 2024.
Mara kadhaa amefafanua kwamba wapo kwenye ndoa rasmi ila bado hawajafanya harusi ya umma.
"Umewahi kufikiria kufanya harusi nyeupe?" shabiki alimuuliza mwezi Novemba mwaka jana.
Mama huyo wa mtoto mmoja alijibu: "Ndiyo. Tunafikiria mwisho wa 2023 au mwanzoni mwa 2024. Mimi ni mpenda ukamilifu kwa hivyo ningependa kuchukua muda kupanga kila undani t ukamilifu,".
Mapema mwaka huu, mwanasosholaiti huyo aliweka wazi kwamba hana mpango wa kuongeza mtoto wa tatu hivi karibuni.
Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba atafikiria kupanua familia yake tena baada ya miaka sita.
Vera Sidika hata hivyo alifichua kuwa mume wake, mwimbaji Brown Mauzo anataka sana wapate watoto kumi pamoja.
"Mume wangu anataka watoto kumi. Kwa upande wangu, sio wakati wowote hivi karibuni. Labda nitaongezea mwingine mmoja baadaye kabisa baada ya miaka sita," alisema.
Wawili hao wamekuwa wakichumbiana tangu mwaka wa 2020 na hivi karibuni wanatarajia mtoto wa kiume pamoja.