Wema Sepetu akiri kuumia moyoni, kujiliwaza na pombe baada ya mamake kumvua nguo hadharani

Alifichua kuwa mpenzi wake Whozu pia aliondoka akiwa amejawa na hasira, jambo ambalo lilimuathiri sana kisaikolojia.

Muhtasari

•Wema alifichua kuwa yeye na mama yake Mariam Sepetu hawakuagana vyema baada ya tafrija hiyo ambayo iligeuka kuwa kinyume na alivyotarajia.

•Alieleza kuwa alikunywa pombe tu katika kipindi ambacho alikuwa akiumia moyoni baada ya tukio hilo lakini baadaye akajiikusanya.

Wema Sepetu na mama yake Mariam Sepetu
Image: HISANI

Aliyekuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu amekiri kuzama kwenye dimbwi la huzuni baada ya kuaibishwa hadharani na mama yake mzazi wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha Tanzania, muigizaji huyo alifichua kuwa yeye na mama yake Mariam Sepetu hawakuagana vyema baada ya tafrija hiyo ambayo iligeuka kuwa kinyume na alivyotarajia.

Sio tu kwamba mama yake aliondoka bila wao kuagana, bali pia mpenzi wake Whozu naye aliondoka nyumbani akiwa amejawa na hasira, jambo ambalo lilimuathiri sana kisaikolojia hadi kufikia hatua ya kutafuta faraja kwa pombe.

“Nilibaki pekee yangu, nikawa kama nimebaki nimechanganyikiwa, sijui nifanye nini na nilikuwa nimepitia maumivu makubwa sana.. nisikufiche nilikunywa pombe kwa hiyo naweza kusema ile damage ya mama ilinifanya mimi kufanya kitu ambacho nilikuwa sitarajii,” Wema Sepetu alisimulia.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz alikuwa akitafuta ushauri na majibu kutoka kwa mchungaji na mshauri maarufu nchini Tanzania.

Alieleza kuwa alikunywa pombe tu katika kipindi ambacho alikuwa akiumia moyoni baada ya tukio hilo lakini baadaye akajiikusanya, akafanya mazungumzo na Mungu na kumwendea mpenzi wake Whozu katika juhudi za kurekebisha uhusiano wake ulioathirika.

“Kwa hakika alikuwa ameaibika (Whozu) kwa namna moja au nyingine. Aibu ni kubwa sana. Hata ndugu zake hawajapenda. Wote wanasema kwamba ile ilikuwa sio sehemu sahihi. Lakini tunarudi kusema mzazi hakosei. Uharibifu umefanyika,” Wema alisema.

Mrembo huyo alikiri kuwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita amekuwa katika hali ya sintofahamu na amekuwa haelewi haswa anajisikiaje.

Mwishoni mwa mwezi Septemba, Bi Mariam alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa karamu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya bintiye  alimkosoa kuhusu uhusiano wake na mwimbaji Whozu akitaja kuwa haukubarikiwa.

Mamake Wema lifichua kuwa alihisi kutoheshimiwa na bintiye na mpenzi wake kwani walikuwa wameweka uhusiano wao hadharani bila hata kutafuta baraka zake. Aliendelea kuongeza kuwa ukiwa mtoto ni jambo la msingi kuwajulisha wazazi wako una uhusiano na nani na kumfahamu mtu ambaye una uhusiano naye.

"Nataka heshima itawale. Nataka wazazi waheshimiwe kama mtoto, lazima umsikilize mzazi wako. Kwa mpenzi ni lazima uje kujitambulisha," alisema Mariam kwa hasira.

Bi Mariam alifafanua kuwa hakuwa akijaribu kuelekeza maisha ya bintiye au kumzuia kupata mapenzi ila alichokuwa akiomba ni heshima tu, bila kulazimika kujua undani wa maisha ya bintiye mtandaoni. Aidha, alishikilia kuwa alikuwa akifanya haya yote kwa sababu ya upendo mkubwa alionao kwa binti yake.